NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
BENKI ya NMB imetoa gawio la Sh. Bilioni 64 kwa serikali kwa mwaka 2025, likiwa ni ongezeko kutoka sh. Bilioni 16 zilizotolewa mwaka jana.
Gawio hilo limetolewa leo Ikulu jijini Dar es Salaam na kupokelewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kupokea gawio na michango kutoka kwa taasisi na mashirika ya umma.
Akitangaza magawio hayo Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema kampuni zingine zilitoa gawio ni PUMA ambao wao wametoa Sh. Bilioni 12 mwaka huu kutoa Bilioni nane walizozitoa mwaka jana.
“Nao Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) wametoa Bilioni 10 mwaka huu kutoa Bilioni 1.3 ambazo walitoa mwaka jana, TIPER nao wametoa Bilioni 5.5 kutoka Bilioni 1.5 za mwaka jana. Hii yote inatokana na mazingira na mahusiano mazuri ya kiuwekezaji na kibishara ambayo yamewekwa na Serikali yako ambayo yamejenga imani kubwa na wabia wenzetu,” amesema Mchechu
Amesema gawio zinatokana pia na kuimarisha Bodi za wakurugenzi kwani idadi ya taasisi na mashirika yasiyokuwa na bodi za wakurugenzi imepungua kutoka taasisi 52 mwaka 2019/2020 hadi kufikia taasisi 28 mwaka huu ikiwa ni ufanisi wa asilimia 46.
“Pia kumekuwa na ongezeko la kampuni za madini ambapo Serikali ina hisa kupitia Msajili wa Hazina kutoka Kampuni 4 mwaka 2019/2020 hadi 12 kwa sasa ikiwa ni ongezeko la asilimia 200. Aidha, tupo mbioni kusaini mikataba mingine 10 mipya,” amesema
Mchechu amesema kumekuwa na kuimarika kifedha kwa mashirika ya umma yaliyokuwa na mitaji hasi na yaliyokuwa yanapata hasara mfululizo, ambapo sasa yameweza kuondokana na utegemezi wa ruzuku ya Serikali na kufanikiwa kutoa gawio.
Ameyataja baadhi ya mashirika hayo ni pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).