NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kuwa utumishi wa dini ni ule unaowasaidia jamii na kuwawezesha wenye mahitaji maalumu kuishi maisha bora huku akilipongeza Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT) kwa kazi wanayofanya ambapo amesema inapeleka ujumbe kwa wale waliojionesha kama watumishi wa dini lakini ukweli ni watumishi wa shetani.
Rais Samia ameyasema hayo leo Juni 5, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa kituo cha watoto wenye mahitaji maalum cha Bagamoyo Diaconic Lutheran, harambee iliyoendeshwa na Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT).
Amesema kanisa la KKKT limeendelea kuonesha kwa vitendo namna ambavyo inashirikiana na serikali katika kusaidia jamii hasa kwenye masuala elimu, afya na ujenzi wa maadili kwa ujumla.
“Mmetukumbusha kuwa kuwalisha wenye njaa, kuwanyesha wenye kiu, kuvika wasiokuwa na nguo na kutembelea wagonjwa ni jukumu letu sote, mbali na hayo nimesikia kwa Katibu Mkuu wa Dayosisi ametaja mambo mbalimbali yanayoyafanywa na Kanisa sasa huu ndio utumishi wa dini na kazi hii mnayofanya inapeleka ujumbe kwa wale waliojionesha kama watumishi wa dini lakini kwa kweli ni watumishi wa shetani,” amesema Rais Samia
Rais Samia amesema utumishi wa dini ni kuwajali wenye wahitaji, kufanya mambo mbalimbali yanayogusa jamii pamoja na kujenga jamii iliyobora yenye maadili na elimu.
Aidha Rais Samia kupitia Ofisi yake ya Rais imechangia kiasi cha Sh. Milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha watoto wenye mahitaji maalumu cha Bagamoyo Diaconic Lutheran.
Kati ya fedha hizo, Rais Samia amechangia Sh. Milioni 100 kama Rais pia ametoa Milioni 50 kama mama kwa watoto hao huku wasaidizi wake wakichangia Milioni 100.
“Ninapoalikwa kwenye mambo makubwa ya kanisa kuna kiwango nimejiwekea kuchangia ambayo ni Sh.Milioni 100 lakini leo kwa maajabu makubwa niwashukuru washauri wangu kama sita hivi au saba na wao wamejikusanya wanakuja na Sh. Milioni 100 lakini baba askofu ulisema watoto hawa wana matumaini makubwa na mimi bibi yao, hivyo nikivaa kofia ya bibi yao nawachangia milioni 50, hivyo ukipiga jumla ni Sh. milioni 250,” amesema Rais Samia