NA ASHRACK MIRAJI,SAME,KILIMANJARO
KATIKA kuendeleza uwajibikaji kwa jamii, taasisi ya kifedha ya SAME KAYA SACCOS imetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa makundi yenye uhitaji katika Wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro. Msaada huo umetolewa kama sehemu ya kuadhimisha mchango wa jamii katika mafanikio ya SACCOS hiyo.
Msaada huo ni mfano bora wa taasisi za kifedha kurudisha kwa jamii wanakotoka.
Kwa mujibu wa Meneja wa SAME KAYA SACCOS, Elvera Mdee, taasisi hiyo imetumia jumla ya Shilingi milioni tano katika kugharamia ununuzi wa bidhaa hizo, ambazo ni pamoja na vyakula, vinywaji, sare za shule , vifaa vya usafi na vifaa vya shule
Walengwa wa msaada huo ni pamoja na hospitali ya Wilaya ya Same, Shule ya Sekondari Chauka iliyopo Hedaru, pamoja na kituo cha kulelea yatima cha Rafiki Children Centre kilichopo mjini Same.
Kila taasisi ilipokea msaada kulingana na mahitaji maalum yaliyobainishwa awali.
Katika hafla ya kukabidhi misaada hiyo, Mdee alieleza kuwa SAME KAYA SACCOS inaamini katika kuijali jamii na kuwa karibu na wananchi, hasa wale walio katika mazingira magumu.
Alisisitiza kuwa mafanikio ya taasisi hiyo hayawezi kufikiwa bila ushirikiano kutoka kwa wananchi wa Wilaya ya Same.
Aidha, alitoa wito kwa taasisi nyingine za kifedha na wafanyabiashara binafsi kujitokeza na kusaidia jamii, hususan katika kipindi hiki ambapo hali ya kiuchumi imekuwa changamoto kwa wengi.
“Tunaamini kwamba kila mmoja wetu ana wajibu wa kusaidia kule tunakoweza. SAME KAYA SACCOS inatambua umuhimu wa mshikamano na upendo kwa jamii,” alisema.
Wazazi, walimu na walezi waliopokea msaada huo kwa niaba ya walengwa walitoa shukrani zao kwa taasisi hiyo, wakieleza kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka na utaongeza ari ya watoto kuhudhuria shule, pamoja na kuboresha huduma za afya na mazingira ya usafi katika maeneo yao.
SAME KAYA SACCOS imekuwa mstari wa mbele si tu katika utoaji wa huduma za kifedha, bali pia katika kuhakikisha kuwa jamii inayowazunguka inanufaika moja kwa moja na mafanikio ya taasisi hiyo. Hii ni sehemu ya dira yao ya kuhakikisha maendeleo jumuishi na yenye uwiano kwa wote