NA JANETH JOVIN
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikijiandaa kufanya Mkutano wake Mkuu wa Taifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, leo Mei 28, 2025, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Makao Makuu mapya ya chama hicho jijini Dodoma.
Gharama za ujenzi wa Jengo hilo linalotarajiwa kuwa na ghorofa tano ni Sh. Bilioni 34.13 ambapo hatua hiyo inayochukuliwa kama ishara ya awamu mpya ya mageuzi ndani ya chama hicho tawala.
Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi, Rais Samia amesema kutimia kwa azma hiyo ya muda mrefu ni ushahidi wa dhamira ya chama kuendelea kuwa jukwaa la watu na dira ya maendeleo.
Amesema walilolikusudia kwa miaka mingi leo limetimia na kusisitiza kuwa CCM ni chama cha maendeleo ya watu, na ndiyo maana wananchi wenyewe wametoa maeneo yao kwa hiari kutoa nafasi ya ujenzi huo.
“Nina furaha kuwa na mimi nimekua sehemu ya utekelezaji wa ujenzi wa jengo hili, aidha uamuzi wa kuhusisha kampuni za Watanzania katika ujenzi huo unaashiria imani ya chama kwa uwezo wa wazawa.
“Tumeamua, tumekubaliana, na sasa tunatekeleza,hii ndiyo maana ya chama,nina imani kubwa kuwa kampuni zetu za ndani ambazo zitajenga jengo hili zitafanya kazi kwa viwango vya juu,” amesisitiza Rais Samia.
Rais Samia amesisitiza kuwa jengo hilo si tu alama ya fahari bali linapaswa kuwa kituo cha kujifunzia uongozi, kukuza vipaji, na kujenga kizazi kipya cha watumishi wa chama wenye weledi na maadili.
Amesisitiza kuwa, “Utendaji mzuri wa chama hauwezi kupimwa kwa jengo zuri pekee, bali kwa namna linavyotumika kukuza viongozi bora wa baadaye, Tunapojenga, lazima tuhakikishe tunajenga heshima ya chama chetu,” amesema Rais.
Katika hatua nyingine , Rais Samia ametangaza kufunguliwa kwa dirisha rasmi la wanachama wa CCM kuchangia kwa hiari ujenzi wa jengo hilo hatua inayotarajiwa kuimarisha ushirikishwaji na umiliki wa wanachama katika miradi ya chama chao.
Ametoa rai kwa Halmashauri Kuu ya CCM kusimamia kwa ukaribu mradi huo ili ukamilike kwa wakati, akisisitiza kuwa chama kinahitaji kusimama kwa miguu yake yenyewe kupitia mshikamano, nidhamu na uwajibikaji wa viongozi na wanachama.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama hicho Dk.Emmanuel Nchimbi amesema kuanza kwa ujenzi wa jengo hilo ilikuwa ni ndoto ya Waasisi wa chama ili kuweka Uhalisia wa Kisasa.
Amesema Makao hayo mapya, yenye ghorofa tano, ni sehemu ya ndoto iliyoasisiwa mwaka 1977 lakini utekelezaji wake umekuwa safari ndefu iliyopambwa na changamoto mbalimbali na kwamba jengo hilo sasa limepewa kipaumbele kikubwa na linalenga kukamilika kabla ya jubilei ya chama mwaka 2027.
“Jengo hili litaakisi sio tu ukubwa wa CCM, bali pia nafasi yake kama kinara wa kuongoza mabadiliko ya kijamii na kisiasa nchini, Fedha za awali shilingi bilioni 8 zipo tayari, kati ya bilioni 34 zinazohitajika hadi kukamilika kwake,” amesema Dk. Nchimbi.
Naye Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, ameshiriki hafla hiyo na kupongeza hatua hiyo ya kihistoria, akisema, “Rais Samia ameacha alama nyingi ndani ya chama chetu,Ujenzi huu ni moja ya vielelezo vya mabadiliko chanya na maono makubwa ya uongozi wa sasa.”amesema
Kutokana na hatua hiyo baadhi ya wanachama wa CCM wamesema kuanza kwa ujenzi wa jengo hilo linaipa sura mpya taswira ya chama, ikiashiria uongozi unaojali urithi wa kihistoria huku ukikumbatia mahitaji ya sasa na kesho.