*WAZIRI DK.GWAJIMA AAINISHA VIPAUMBELE VITANO
NA MWANDISHI WETU , DODOMA
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk. Dorothy Gwajima ameainisha Vipaumbele vitano kwa utekelezaji wa mwaka wa fedha 2025/2026.
Waziri Gwajima ameainisha hayo wakati akiwasilisha Bajeti hiyo kwa Mei 27, 2025 bungeni jijini Dodoma.
Katika hotuba yake, ameeleza kuwa, Wizara kupitia Idara na Taasisi zilizo chini yake zitatekeleza vipaumbele hivyo ambavyo ni: kukuza Ari ya jamii kushiriki katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ngazi ya msingi, kuratibu na kuimarisha utoaji wa huduma za ustawi na maendeleo ya jamii, kutambua pamoja na kuratibu maendeleo ya ustawi kwa Makundi Maalum.
Vipaumbele vingine ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia katika Taasisi na Vyuo vya Ustawi na Maendeleo ya Jamii na kuimarisha mazingira ya ushiriki na mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya Taifa.
Aidha, Waziri amesema, Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kuhamasisha na Kusimamia Maendeleo katika Ngazi ya Msingi kwa mwaka 2022/23 – 2025/26 ambao, unalenga kuwawezesha wananchi kuwa kitovu cha maendeleo na kuchochea mageuzi ya kifikra, mtazamo na kiutendaji kwa timu ya wataalam ngazi ya msingi ili kuboresha utendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kuhusu baadhi ya maeneo ya utekelezaji uliopita kwa ufupi amesema ilikuwa ni pamoja na kuhakikisha Watoto wanalindwa na ukatili kwa kuratibu na kusimamia Kampeni ya Taifa ya Usalama wa Mtoto Mtandaoni katika Mikoa 26 ya Tanzania Bara kwa lengo la kuelimisha Wazazi au Walezi na Watoto wenyewe kuhusu Usalama wa Mtoto anapokuwa anatumia mitandao.
Vilevile amesema, utekelezaji pia ulihusu kuanza kwa programu ya kuwawezesha Wafanyabiashara ndogondogo ambapo, kwa sasa jumla 601 wamekopeshwa mikopo yenye thamani ya Sh. Bilioni 1.1 na zoezi hilo linaendelea na mikopo hii ni kwa wanawakena wanaume mtu mmoja mmoja.
Kwa kirefu amesema, hotuba ya bajeti hiyo inapatikana kwenye tovuti ya wizara ya www.jamii.go.tz
Bajeti hiyo ya Sh. 76,057,153,000.00 imepitishwa kwa sauti moja na Wabunge wote.