NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
WAKILI wa Kujitegemea wa Mahakama Kuu Peter Madelekaamejiunga na Chama cha ACT Wazalendo akitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Wakili Madeleka amepokelewa na Makamu Mwenyekiti Bara wa ACT-Wazalendo Isihaka Mchinjita akiambatana na Katibu Mkuu wa chama hicho Ado Shaibu Mei 20,2025.
Mara baada ya kukabidhiwa kadi yake ya uanachama, Wakili Madeleka amesema ameamua kujiunga ACT Wazalendo ili kutumia uzoefu na uwezo wake wa kitaaluma kwenye nyanja ya sheria, haki za binadamu na demokrasia kutoa mchango wake katika ujenzi wa taasisi imara za kisasa, hususani ACT Wazalendo, ili kuimarisha upinzani dhidi ya CCM.
‘’Nimejiunga ACT Wazalendo ili kuimarisha nguvu za upinzani na hivyo kutoa fursa kubwa ya
matumaini kwa watanzania kwamba muda si mrefu tutafika kule tunakotaka kufika. Hitaji la kuwa
na maendeleo ya kisiasa, hitaji la kuwa na demokrasia katika nchi yetu, hitaji la kuwa na utawala unaoheshimu haki za binadamu, ni vita kama zilivyo vita nyingine. Vita yeyote ile inapopiganwani lazima ipiganwe kwa njia nyingi, siyo kwa njia moja, huwezi kuweka mayai yote kwenye kapu moja,” amesema Wakili Madeleka
Awali, Makamu Mwenyekiti Bara Isihaka Mchinjita akimkaribisha Wakili Madeleka amemwelezea kuwa ni miongoni mwa wawakili na mwanaharakati nguli na mwenye ujasiri mkubwa wa kupigania haki na demokrasia nchini ambaye rekodi yake imejipambanua.
Alisema ni Wakili na Mwanaharakati anayeguswa na kutetea kila kundi la kijamii bila ubaguzi, na kwamba hilo limedhihirishwa na baadhi ya kesi
alizowahi kusimamia na kushinda ikiwemo kesi ya ugaidi iliyokuwa ikiwakabili baadhi ya Masheikh mkoani Arusha.