NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Tanzania imewasilisha pendekezo la kuanzisha uhusiano wa kibunge na Serikali ya Finland ili kuwa na jukwaa la kuzungumzia yanayotokea hapa nchini.
Rais Samia ameyasema hayo jana Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo rasmi baina yake na Rais wa Finland Alexander Stubb ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku tatu.
Aidha Rais Samia amesema nchi hizo mbili zimekubaliana kuhusu umuhimu wa kuendelea mashauriano ya kidiplomasia na kuratibu ziara za biashara za wadau wa sekta binafsi kati ya nchi zao ili kukuza zaidi ushirikiano wa kiuchumi.
“Kwa muda mrefu Finland amekuwa mbia mkubwa wa maendeleo hapa nchini kwa hivyo kadri Tanzania inavyokua kiuchumi ni matamanio yetu kuona wawekezaji kutoka nchi rafiki ya Finland wanashirikiana na Tanzania kuchochea biashara na uchumi baina ya nchi zetu na ndani ya Afrika kwa ujumla,” alisema Rais Samia
Hata hivyo alisema katika mazungumzo yake na Rais Stabb yalijikita katika maeneo mbalimbali yakiwemo sekta ya misitu, biashara, uwekezaji, madini, utalii, elimu, uwezeshaji wanawake, Tehama na uhamirishaji wa tekonolojia.
Alisema maeneo hayo kwa muda mrefu Finland imekuwa mbia wao katika kuyaendeleza na kwamba wote wamekubaliana kuwa kuna fursa kubwa ya kukuza zaidi ushirikiano katika maeneo hayo na kueleza utayari wao wa kutumia fursa hizo kwa manufaa ya mataifa hayo mawili.
Rais Samia alisema katika sekta ya misitu, Finland imekuwa ikiwasaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya usimamizi wa uhifadhi wa mazingira nchini na kwamba katika ziara hiyo Rais Stubb atazindua mpango wa Forland unaolenga kuzijengea uwezo taasisi za mafunzo kwenye sekta ya misitu nchini.
“Kama mnavyofahamu nchini kwetu tuna mkakati wa taifa wa Nishati safi ya kupikia ambao unalenga kuongeza matumizi ya nishati safi na kulinda mazingira, lengo letu ni kufanya asilimia 80 ya jamii ya kitanzania kutumia nishati safi ifikapo 2034 ili kulinda msitu yetu.
“Hivyo nimeikaribisha Serikali ya Finland kushrikiana na Tanzania katika kufanikisha mkakati huo unaolenga kuimrisha ustawi wa afya wa watu na mazingira kwa ujumla,” alisema Rais Samia
Hata hivyo Rais Samia alisema wameikaribisha sekta binafsi ya Finland kushirikiana na Tanzania katika kuwekeza kwenye kuongeza thamani madini yanayopatikana hapa nchini ili kuzalisha bidhaa kwa ajili ya masoko ya nje.
“Pia kwenye mazungumzo yetu tumeeleza dhamira ya kuimarisha uhusiano wetu kwa kuongeza maeneo mengine mapya ya ushirikiano katika sekta muhimu ikiwemo uchumi wa buluu, nishati na elimu kwa manufaa ya watu wetu.
“Nimemshirikisha pia kuhusu nia yetu ya kuongeza idadi ya watalii wanaotoka Finland kuja kutembelea Tanzania na nimemwambia mwaka jana kulikuwa na watalii 5067 na robo ya kwanza ya mwaka huu tuna watalii 1276, hivyo tumeomba tushirikiane katika kukuza utalii kwenye janja tofauti,” alisema Rais Samia
Kuhusu Sekta ya Elimu, Rais Samia alisema wameomba kuimarisha ushirikiano katika sekta hiyo na kubadilishana ujuzi katika eneo la ufundi stadi, mafunzo ya kidigitali na kuwajengea uwezo walimu pamoja pia walijadili mustakabali wa ushirikiano kupitia Taasisi ya Uongozi.
Kwa upande wake Rais Stubb alisema suala la amani duniani ni muhimu ili kuimarisha uhusiano wa mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania na Finland, na kwamba pande mbili zikikidhana basi amani hutoweka.
Alisema katika majadiliano aliyoyafanya na Rais Samia waligusia pia utaratibu wa kiulimwengu wa jinsi siasa za kidunia zinavyobadilika na kwamba Finland itaangalia namna ya kusaidia kulikuza bara la Afrika ili liweze kuku ana kupata sauti kubwa katika ngazi ya kimataifa.
Rais Stubb yupo nchini kwa ziara ya siku tatu kwa mwaliko wa Rais Samia, hakiwa nchini Rais Stubb atashiriki matukio mbalimbali ikiwemo semina kuhusu urithi wa Hayati Mariti Ahtisari Rais Mstaafu wa Finland na Mwanadiplomasia mbobezi aliyeshika nafasi mbalimbali ikiwemo mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Nchini Namibia na Kosovo
Pia atahutubia jukwaa la wafanyabiashara wa Tanzinia a Finland litakalofanyka Mei 16, 2025 litakalojadili fursa za kiuchui na biashara baina ya nchi hizi mbili.