NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
SERIKALI ya Tanzania na Msumbiji zimetiliana saini mkataba wa kubadilishana wafungwa baina ya nchi hizo mbili.
Aidha Serikali hizo mbili pia zimeingia makubaliano ya kubadilishana wanafunzi wanaotoka katika nchi zao kwa ajili ya kusoma na kupata elimu katika ngazi mbalimbali.
Mikataba hiyo yote imesainiwa leo Mei 8, 2025 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya siku tatu ya Rais wa Msumbiji hapa nchini, Daniel Chapo.
Katika mkataba wa kwanza wa kubadilishana wafungwa umetiwa saini na Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji, Maria Dosantos Lucas kwa niaba ya nchi hiyo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa Tanzania, Innocent Bashungwa.
Kutokana na mkataba huo nchi hizo mbili zitakuwa na uwezo wa kubadilishana wafungwa kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine.
Hata hivyo katika mkataba wa kubadilishana wanafunzi umesainiwa pia Ikulu Jijini Dar es Salaam, kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa
Msumbiji, Lucas kwa niaba ya nchi hiyo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabiti Kombo kwa upande wa Tanzania.
Kutokana na mkataba huo, nchi hizo mbili zitakuwa na uwezo wa kubadilishana wanafunzi kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine.
Vilevile Serikali ya Tanzania imeingia makubaliano na Serikali ya Msumbiji ya kushirikiana katika kukuza na kuendeleza utamaduni baina ya nchi hizo mbili.
Hati ya makubaliao hayo nao imesainiwa leo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji, Lucas kwa niaba ya nchi hiyo na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi kwa niaba ya Tanzania.
Chini ya makubaliano hayo, nchi hizo mbili zitakuwa na uwezo wa kubadilishana mambo mbalimbali ya kiutamaduni.
Pia Serikali ya Tanzania na Msumbiji wamesaini hati ya makubaliano na ushirikiano kati ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) na Mamlaka ya Taifa ya Kudhibiti Dawa ya Msumbiji.