▪️Waziri Mavunde aelekeza mchakato wa mabadiliko ya sheria kuanza.
▪️Aelekeza kanuni kubadilishwa kupunguza tozo kwa hekta kufikia 20,000.
▪️Wazalishaji Chumvi wampongeza Rais Dk. Samia S. Hassan kwa ujenzi wa kiwanda cha Chumvi Mkoani Lindi
▪️Serikali kuwezesha wazalishaji chumvi kumiliki viwanda vya kuchakata chumvi
NA MWANDISHI WETU,DODOMA
SERIKALI ipo mbioni kutambulisha Leseni mpya ya uzalishaji wa chumvi ili kuiondoa chumvi katika kundi la madini mengine na hivyo kuchochea ukuaji wa tasnia ya uzalishaji chumvi nchini Tanzania.
Hayo yamesemwa leo Mei 1,2025 Jijini Dodoma wakati wa Kikao cha Waziri wa Madini Anthony Mavunde na Uongozi wa Chama cha Wazalisha Chumvi Tanzania(TASPA),kikao ambacho kimelenga kuboresha sekta ya madini kupitia tasnia ya chumvi.
“ Mh. Rais Dk. Samia S. Hassan ametupa maelekezo mahsusi kuwezesha wachimbaji wa madini na wazalishaji wa madini chumvi nchini ili kuchochea ukuaji wa sekta ya madini.
Serikali imesikia kilio chenu cha muda mrefu cha uwepo wa Leseni moja ya uzalishaji wa Chumvi ambayo itasaidia kumuendeleza mzalishaji chumvi kwa kupunguza gharama za uzalishaji na kuyaondoa madini chumvi katika kundi la madini mengine.
Naelekeza kuanza mara moja mchakato wa mabadiliko ya sheria ili kuruhusu uanzishwaji wa Leseni maalum ya uzalishaji chumvi ambayo pia tozo yake kwa hekta iangaliwe upya kufikia 20,000 kutoka kiwango kilichopo sasa.
Dhamira ya serikali ni kuona wazalishaji wa chumvi wanaongeza tija na kufikia hatua ya kumiliki viwanda vya uchakataji na usafishaji chumvi nchini ili chumvi yetu iwe yenye ubora na shindani” amesema Mavunde
Aidha Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Mhandisi Yahaya Samamba ameipongeza TASPA kwa kazi ya kuwaendeleza na kuwasimamia wazalishaji chumvi na kuahidi ushirikiano wa kutosha kutoka Wizarani katika utatuzi wa changamoto za wanachama wake.
Akitoa maelezo yake,Mwenyekiti wa TASPA Hawa Ghasia ameipongeza wizara ya madini kwa utaratibu wa kuwasikiliza wadau na kutafuta suluhisho ya changamoto zao na kutumia fursa hiyo kumpongeza kipekee Rais Dk. Samia S. Hassan kwa kusikia kilio cha wazalishaji wa chumvi kwa kujenga kiwanda cha Kuchakata na kusafisha chumvi kinachojengwa mkoani Lindi na Shirika la Madini la Taifa(STAMICO).