*SERIKALI YAAHIDI KUENDELEA KUTOA FEDHA KWAAJILI YA UWEZESHAJI
NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
MAKAMU wa RAIS Dk. Philip Mpango ametoa wito kwa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuhakikisha Tuzo za Taifa ya Mwalimu Nyerere za Ubunifu zinakuwa endelevu na Serikali itaendelea kutoa fedha Kwa ajili ya uwezeshaji.
Hayo yamebainishwa Aprili 13,2025 wakati wa hafla ya utoaji tuzo hizo na Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega , akimwakilisha Makamu wa Rais Dk.Mpango.
Amesema tuzo hizo ni muhimu kwa kuwa zinaenzi Kwa vitendo yaliyofanywa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambaye alikuwa mtunzi wa mashairi na mtafsiri wa riwaya mbalimbali zilizokuwa kwa lugha ya kiingereza na kuziweka kwenye kiswahili.
Pia ameweka wazi kuwa tuzo hizo zimekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza Kiswahili kutokana kwamba moja ya masharti ya utunzi ni kutumia lugha ya kiswahili.
Aidha ameongeza kuwa Kwa sasa lugha ya Kiswahili inazidi kuvuka mipaka kwa mataifa mbalimbali kuingia mikataba na Tanzania kufundisha katika nchi zao.
Ameongeza kuwa kwa kazi ambazo zinapata nafasi ya miswada yao kuchapishwa inasaidia kuinua lugha ya kiswahili kutokana na kutumika kwenye shule mbalimbali nchini na kuwa sehemu ya kufundishia.
Waziri Ulega kwa niaba ya Makamu wa Rais amewaasa washindi wa nafasi ya nne hadi ya 10 ambao walitunukiwa vyeti vya ushiriki kutokata tamaa kwani bado wana nafasi ya kufanya vizuri zaidi katika tuzo zijazo kwakuwa tayari wamepata uzoevu Kwa kutambua mashindano hayo yanataka vigezo gani ili ufanikiwa kushinda.
Naye Mhadhiri Mwandamizi, Mtunzi na Mchoraji maarufu kutoka Chuo Kikuu Cha Sultan Qaboos, Muscat nchini Oman, Prof. Ibrahim Noor Shariff, amefafanua kwamba kwa sasa Kiswahili kilipofika huwezi kumteta mtu kwani unaweza kudhani mtu aliye karibu yako hajui kiswahili kumbe la hasha na hapo ndipo unapoaibika.
“Pongezi kwa waandaaji wa tuzo hizo Kwani zinamchango mkubwa katika kukuza lugha ya Kiswahili na zinatengeneza vipajj vya watungi katika nyanja ya ushauri, riwaya nk” amesema.
Pia alimuomba mgeni rasmi kufikisha salamu zake Kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuenzi Kiswahili kwa uwezeshaji wa tuzo hizo ambazo ni Tunu ya Taifa.
Aneth Komba, Mkurugenzi Mkuu wa TET, amesema huu ni msimu wa tatu tangu tuzo hizo kuanzishwa na zimekuwa na mafanikio kwa watungi kuongezeka.
“Pia nimshukuru Rais Samia kwa jitihada zake katika kuwezesha tuzo hizo uendelea kufanyika ambazo zinatambua mchango wa Waandishi Bunifu,” amesema.
Ameongeza kuwa mchakato wa tuzo zijazo zinaanza sasa baada ya msimu wa tatu kukamilika na watatoa utaratibu wakati wowote kuanzia sasa.
Penina Mlama, ambaye ni Mwenyekiti wa Jopo la Majaji wa tuzo hizo, amesema kwamba ni jambo jema kuona aina za tuzo zinaongezeka ambapo awali zilikuwa mbili nazoi ni riwaya na ushairi na sasa zimefika nne zikiwemo hadithi za
watoto na tamthilia.
Washindi wa kwanza katika kila kipengere wamekabidhiwa mfano wa hundi ya shilingi mil 10 kila mmoja na washindi wa pili katika kila kipengele amepatiwa mfano wa hundi ya
Sh.Mil 7/- na washindi watatu wamepatiwa mfano wa hundi ya Sh.Mil 5/- kila mmoja.