NA MWANDISHI WETU,KAKONKO,KIGOMA
MAHAKAMA ya Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, katika Shauri la Uhujumu Uchumi namba 2735/2025 – mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kakonko Ambilike Kyamba na Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya TAKUKURU (M) Kigoma Jackson George Lyimo, imewatia hatiani Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kakonko Mhandisi. Benjamin Mjuni Brighton (37) na wenzake wawili.
Wengine waliotiwa hatiani ni Fundi Sanifu wa RUWASA Wilaya ya Kakonko Faraja Charles Kalokola (27) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Chiganda Construction Limited Johansen Muganyizi (46) ambao kwa pamoja walishtakiwa kwa makosa ya Matumizi ya Nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri, Kujipatia Manufaa, Ubadhirifu na Ufujaji, Matumizi Mabaya ya Mamlaka pamoja na Ushawishi kinyume na vifungu vya 22, 23 (1), 28 (1), 31 na 33 vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura namba 329 Marejeo ya mwaka 2022 ikisomwa pamoja na aya ya 21 ya jedwali la kwanza, kifungu cha 57(1) na kifungu 60(2) vya Sheria ya Udhibiti wa Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa Sura namba 200 Marejeo ya Mwaka 2022.
Washtakiwa wamehukumiwa kulipa faini ya sh. 4,000,000/-na kurejesha sh. 53,922,660/-zilizofanyiwa ubadhirifu.