NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amebainisha kuwa Mashirika 31 ya umma yanayofanya biashara yamepata faida katika kipindi hicho, likiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
CAG Kichere amebainisha hayo leo Machi 27, 2025 wakati akiwasilisha Ripoti ya Ukaguzi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa mwaka 2023/2024 mbele ye Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu Dar es Salaam.
Kichere amesema TPDC lilipata faida ya Sh. Bilioni 248.75, NHC Bilioni 242.9, na TPA Bilioni 140.48.
Aidha Kichere, amependekeza kampuni tanzu ya TANESCO inayotengeneza nguzo za umeme za zege ivunjwe kwa kuwa imeshindwa kutekeleza majukumu yake tangu ilipoanzishwa. Badala yake, shughuli zake zifanywe na idara ndani ya TANESCO.
Ameeleza kuwa fedha nyingi zinatumika kulipa gharama za kawaida na kwa wazabuni wa nje wanaotengeneza nguzo,badala ya kampuni hiyo kutekeleza jukumu lake.
“Zaidi ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, bado haijaanzisha uzalishaji wa nguzo wala kuwa na maabara yake ya ndani, hali inayoiweka katika utegemezi wa huduma kutoka nje. kampuni ilianzishwa kwa lengo la kuzalisha na kupima ubora wa nguzo za umeme nchini na katika mwaka wa fedha 2023/2024, ilipokea bilioni 6 kutoka TANESCO.
“Bilioni 4 zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda na maabara ya kupima ubora wa nguzo, huku bilioni 2 zikielekezwa kwenye gharama za undeshaji. Hata hivyo, fedha nyingi zilitumika kulipa gharama za kawaida na wazabuni wa nje wanaotengeneza nguzo badala ya kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake,” amesema Kichere.