NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ameyataja Mashirika ya Umma yaliyopata hasara za mabilioni ya fedha katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024.
Kichere ameyataja mashirika hayo kuwa ni Shirika la Reli Tanzania (TRC) ambalo limepata hasa ya Sh. Bilioni 224, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) Bilioni 91.8, Shirika la Mawasilinao Tanzania (TTCL)
Akizungumza leo Machi 27, 2025 wakati akiwasilisha Ripoti ya Ukaguzi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa mwaka 2023/2024 mbele ye Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu Dar es Salaam, Kichere amesema TRC imepata hasara hiyo ya Bilioni 224, ikilinganishwa na hasara ya Sh.Bilioni 102 mwaka uliopita.
Amesema miongoni mwa sababu zilizochangia hali hiyo ni uhaba wa vichwa vya treni na mabehewa, pamoja na mvua kubwa zilizosababisha kufungwa kwa njia za reli kwa miezi minne na kwamba hasara hiyo imetokea hadi Juni 30,2024, kipindi ambacho Reli ya Kisasa (SGR) ilikuwa bado haijaanza kufanya kazi rasmi.
Aidha, Kichere amesema kuwa TRC ilipokea ruzuku ya Sh. Bilioni 29.01 kutoka Serikalini, ambayo ilipunguza kiwango halisi cha hasara na kwamba bila ruzuku hiyo, TRC ingepata jumla ya hasara ya Sh. Bilioni 253.
Kichere amesema kwa upande wa ATCL kwa mwaka wa fedha 2023/24, imepata hasara ya Sh. Bilioni 91.8 ikiwa ni ongezeko la asilimia 62 kutoka Sh. Bilioni 56.6 mwaka uliopita.
“Hasara hiyo inatokana na gharama kubwa matengenezo ya ndege na hitilafu za injini ambapo ndege za Airbus zilikaa muda mrefu bila kufanya kazi zikisubiri injini. Pia kampuni ilitumia Sh. Bilioni 99.8 ikiwa ni ruzuku kutoka serikalini endapo isingepewa ruzuku hiyo kampuni ingepata hasara halisi ya Sh. Bilioni 191.6,” amesema
CAG Kichere amependekeza kampuni ishirikiane na Serikali katika kufanya utafiti wa njia bora zaidi za uendeshaji wa ndege kwa kuzingatia masuala ya kifedha na kiuchumi kuongeza ufanisi wa uendeshaji.
Kwa upande wa TTCL, amesema lilipata hasara ya Sh. Bilioni 27.7 mwaka wa fedha wa 2023/2024 na kwamba ongezeko hilo ni kutoka Sh. Bilioni 4.32 ya hasara kwa mwaka uliopita.
“Hasara hii ya mwaka huu inachangiwa na ongezeko la gharama baada ya kuhamishiwa Mkongo wa Taifa na Kituo cha Taifa cha Data. Napendekeza fedha za kulipa madeni ya Mkongo wa Taifa yatoke kwenye mfumo wa hazina,” amesema