NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) imesema kutoka na operesheni mbalimbali za uchunguzi walizofanya kwa mwaka wa fedha 2023/24 imefanikiwa kuokoa kiasi cha Sh. Bilioni 30.19.
Hayo yamebainishwa leo Machi 27, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Crispin Chalamila wakati akiwasilisha ripoti ya utendaji wa taasisi hiyo ya mwaka 2023/2024 kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Amesema baadhi za chunguzi zilizofanikisha uokoaji huu ni mikopo isiyorejeshwa katika Benki ya Maendeleo (TIB) kiasi cha Sh. Bilioni 6.6 ambayo ilitolewa bila kuzingatia utaratibu na vigezo kwa Kampuni Amboni Sisal Properties Ltd ya Tanga.
Chalamila amesema chunguzi zingine zilizofanikisha uokoaji wa fedha hizo ni ushuru uliokusanywa katika maeneo ya masoko, minada na maneneo mengine katika halmashauri ya Ilala kiasi cha Sh. Bilioni 6.8 wakusanyaji hawakuwasilisha fedha hizo benki ambapo zimerejeshwa na kuwekwa kwenye akaunti ya mfuko mkuu wa halmashauri hiyo.
“Chunguzi nyingine ni ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo katika halamshauri kiasi cha Sh. Bilioni 3.1 kati ya fedha hizo kiasi cha Sh. Bilioni 1 fedha taslimu zilirejeshwa kwemye akaunti za halmashari na sh. Bilioni 2 ilidhibitiwa sambamba na vifaa kurejeshwa katika miradi husika,” amesema
Hata hivyo amesema ukwepaji kodi wa Sh. Bilioni 2.04 kati ya fedha hiyo Sh. Milioni 281.44 ilikuwa ni fedha ya kodi iliyokwepwa kulipwna wafanyabiashara mbalimbali wa mkoani Kigoma na pia Takukuru imeokoa kiasi cha Sh.Bilioni 2.15 iliyotokana na ukwepaji wa kidi ya zuio.
Aidha amesema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la Transparency imeonesha kuwa Tanzania ni nchi ya pili kuwa na kiwango cha chini zaidi cha vitendo vya rushwa kati ya nchi kumi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Kwa mujibu wa ripoti hiyo Tanzania imeendelea kuimarika katika kupunguza rushwa na kwamba katika kipindi cha mwaka 2014/24 inaonesha kwamba Tanzania imepanda kwa alama kumi na ni mojawapo ya nchi nne za kusini mwa Jangwa la Sahara yenye kuzidi kuimarika kupambana na vitendo vya rushwa,”
Kuhusu Halmashauri
Chalamila amesema uchunguzi walioufanya umebaini halmashauri 52 kati ya 101 zinakata kodi ya zuio kutoka kwa wazabuni mbalimbali ambapo halmashauri 41 kutoka kwenye hizo 52 zinawasilisha kodi kamilifu huku 11 zikiwasilisha kodi pungufu.
Amesema hali hiyo imesababishwa na usimamizi hafifu, kutowajibika kwa halmashauri, kutokuwa na taarifa za kutosha kuhusu kinachotakiwa kupokelewa kutoka kwenye Halmashauri hizo.
“Kilichosababisha kingine ni halmashauri kutokuwa na kumbukumbu sahihi za hundi za kodi za zuio zilizoidhinishwa na kutokuwepo kwa mfumo wa pamoja unaoratibu utekelezaji wa miradi ngazi ya halmashauri, jambo ambalo linaipa TRA ugumu wa kuratibu kodi ya zuio na hivyo kutoa mwanya wa ufujaji wa mapato husika,” amesema
Mbali na hayo, Chalamila amesema kuwa wamebaini uzingatiaji wa mkataba wa huduma kwa mteja wa Wizara ya Ardhi wa mwaka 2020 upo chini ya asilimia 50.
“Uchambuzi umefanyika katika masuala kadhaa ikiwemo katika mchakato bwa utoaji wa huduma za ubadilishaji wa matumizi ya ardhi, kuomba na kupewa kiwanja, utoaji wa hati milki za ardhi, uhamishaji wa milki ya ardhi na upitishaji wa vibali vya ujenzi wa nyumba za kawaida,” amesema
Chalamila amesema uchambuzi huo pia umebaini kuwa changamoto zinazokwamisha utoaji wa huduma katika sekta ya ardhi kama ilivyoelekezwa katika mkataba wa huduma kwa mteja ni pamoja na upungufu wa rasilimali watu, fedha na vitendea kazi katika utoaji wa huduma za ardhi na mifumo ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za ardhi kutosomana