NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere amesema hadi kufikia Juni 30, 2024 deni la Taifa lilifikia Sh. Trilioni 97.35, ambapo kiasi hicho kimeongezeka kutoka kiasi cha Sh. Trilioni 82.25 kilichoripotiwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Kichere ameyasema hayo leo Machi 27, 2025 wakati akiwasilisha ripoti ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2023/2024 mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa deni hilo ni sawa na ongezeko la Sh. Trilioni 15.1 na kwamba deni hilo linajumuisha deni la ndani la Sh. Trilioni 31.95 na deni la nje la Sh. Trilioni 65.4 na kwamba deni hilo bado ni himilivu.
“Tathmini ya uendelevu wa deni la Taifa imebaini kuwa deni la Taifa bado ni himilivu kwa kuwa viashiria vikuu vinaonesha thamani halisi ya deni la nje ni asilimia 23.6 ya pato la Taifa chini ya ukomo wa asilimia 40,” amesema Kichere
Amesema deni la jumla ni asilimia 41.1 ya pato la Taifa chini ya ukomo wa asilimia 55 na kwamba malipo ya deni hilo kwa kutumia mapato ya nje ni asilimia 127.5 chini ya ukomo wa asilimia 180 na kwamba malipo ya deni la Taifa kwa kutumia mapato ya Serikali ni asilimia 14.5 chini ya ukomo wa asilimia 18.
Hata hivyo Kichere ameridhishwa na namna ambavyo mapendekezo ambayo ofisi yake imekuwa ikiyatoa kutokana na ripoti za ukaguzi yakifuatiliwa na kufanyiwa kazi.
Kichere amempongeza Katibu Mkuu kiongozi Dk. Moses Kusiluka kwa kuonesha umahiri wa kuratibu mchakato wa kusimamia utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi kupitia kwa makatibu wakuu ambao ni Maofisa Masuhuli.
“Katika ripoti ya ukaguzi ya miaka ya nyuma nilitoa mapendekezo kadhaa yaliyokusudia kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma na kuboresha ukusanyaji wa mapato nchini, nimeona serikali ikifanyia kazi mapendekezo niliyoyatoa katika ripoti zangu za ukaguzi ambapo Ofisi ya Rais imekuwa ikitoa miongozo mingi juu ya kushughulikia mapendekezo hayo,” amesema Kichere
Mwenendo wa hati za ukaguzi
Aidha Kichere amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 ametoa jumla ya hati 1301 ikiwa ni ongezeko la hati 92 ikilinganishwa na 1209 zilizotolewa mwaka wa fedha 2022/2023 na kwamba kati ya hizo zilizotolewa mwaka huu 220 zinahusu Tamisemi, 218 zinahusu mashirika ya umma, 513 serikali kuu, 19 vyama vya siasa na 332 zinahusu miradi ya maendeleo.
Amesema kati ya hati hizo safi ni 1295 sawa na asilimia 99.5, zenye shaka tano sawa na asilimia 0.4 na mbaya ni moja sawa na asilimia 0.1 na kwamba kwa ujumla hati za ukaguzi wa hesabu zinaonesha utayarishaji wa hesabu unadhirisha na kuimarika na kwa kiasi kikubwa unazingatia taratibu na kanuni za uandaaji wa hesabu za kimataifa.