NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema kuwa nishati ya umeme siyo anasa katika maisha ya watu bali itakuwa ndio injini ya kwanza ya kubadilisha uchumi wa nchi na maisha ya watanzania kwa ujumla.
Dk. Biteko ameyasema hayo leo Machi 4, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la kuhamasisha matumizi ya nishati ya kupikia kwa umeme lililoandaliwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Biteko amesema ni ukweli uliyowazi kuwa umeme siyo hanasa bali ni injini ya kubadilisha uchumi hivyo anawaomba wanawake hasa wa Tanesco kuambiana ukweli na kumkemea mtu yeyote miongoni mwao anayemtafuta mteja na kumuomba rushwa ili amuunganishie4 umeme.
“Tuwakemee watu hawa kwa nguvu zetu zote ili watanzania wapate umeme wa uhakika kwa sababu serikali yao inawekeza fedha nyingi kwa ajili ya kuwapatia umeme, ninaamini wakinamama wakiamua katika shirika hili tutakuwa na shirika bora,” amesema Dk. Biteko
Aidha amewataka wanawake waliopo Tanesco kuwa wa kwanza kubadilika kabla ya watu wengine kwa kutumia nishati safi ya kupikia ya umeme.
“Siku moja nitaamua kumtembelea mmoja wa watumishi ili kuona mnapikaje huko je mnatimua majiko ya umeme, si huwa mnaodha na kuodhesha kwenye sherehe zenu, msishangae nikaja na kupitiliza hadi jikoni kuangalia mnapikaje, maana tusihubiri injili ambayo sisi hatuiishi, tuanze sisi kupikia nishati safi nak ama jiko kwako una mbadala wa mkaa toa tafuta mkaa mabadala,” amesema Biteko
Dkt. Biteko amesema kuna baadhi ya watu wanaamini kupika kwa kutumia umeme ni gharama kubwa hivyo umeme kazi yake ni kuzima na kuwasha taa tu, jambo ambalo amesema si kweli hivyo watanzania wanapaswa kuondokana na dhana hiyo.
“Niwatoe wasiwasi kuna majiko mbalimbali sasa hivi ambayo yanatumia umeme ambapo Unit moja unaweza kupikia kwa zaidi ya saa moja ambayo thamani yake haizidi Sh. 350. Hivyo tutaendelee kutoa elimu kwa jamii kuwa nishati ya umeme ni nafuu na rahisi kutumia,” amesema
Hata hivyo Dk. Biteko amesema kuwa kupitia mfuko wa Nishati safi ya kupikia, Serikali itahakikisha kuwa wanawake wanapata mikopo yenye riba nafuu ili waweze kushiriki kikamilifu katika biashara za nishati safi.
Pia, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa Sera na Sheria mbalimbali zinakuwa rafiki kwa wawekezaji wa nishati safi ya kupikia ili waweze kushiriki kikamilifu katika biashara ya nishati safi ya kupikia.
Aidha Dk. Biteko amempongeza Mkurugenzi wa Tanesco kwa kuanza kutoa fursa sawa kwa wanawake kushika nafasi za juu za uongozi ndani ya Tanesco kwani kwa muda mrefu nafasi za juu za uongozi hasa wakurugenzi katika shirika hilo zimekuwa zikishikwa na wanaume.
“Katika wakurugenzi wote waliopo Tanesco 12 kati ya hao wanne ni wanawake, nimpongeze Mkurugenzi wa Tanesco katika hili kwa kuanza kutoa fursa sawa, hata hivyo bado tunakazi ya kufanya ya kuhakikisha tunatoa fursa kwa wanawake kushika nafasi za juu za uongozi,” amesema.
Naye, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amewataka watanzania hususan wanawake kuendelea kuiunga mkono ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watanzania wote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Gissima Nyamo – Hanga amesema kuwa Serikali imeweka msukumo katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia nishati ya umeme kwa kuwa ni nafuu zaidi na imefika kila mahali nchini.
Amesema ni muhimu wananchi wakatumia majiko ya umeme ili waweze kuokoa muda na kwamba ajenda ya nishati safi ya kupikia ni ya kipaombele na imezungumzwa sana hivyo Tanesco inayowajibu wa kuhakikisha ajenda hiyo inatekelezwa.
Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO, Balozi Zuhura Bundala amesema kuwa wanawake ndio wahusika wakuu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema nishati safi ya kupikia ina gharama nafuu na ni rahisi kwa matumizi.