* Kushiriki Mikutano ya Kimataifa na Wiki ya Nishati ya India
* Mawaziri wa Nishati, Watunga Sera na Wavumbuzi wa teknolojia za
Nishati kukutana
NA MWANDISHI WETU,INDIA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko leo
Februari 11, 2025 amewasili nchini India kwa ajili ya kushiriki
mikutano mbalimbali ya kimataifa ya nishati ambayo inaenda sambamba na
Maadhimisho ya Tatu ya Wiki ya Nishati ya India mwaka 2025 (India 3rd
Annual Energy Week) kuanzia Februari 11 hadi 14,2025.
Katika Uwanja wa Kimataifa wa Indira Gandhi, jijini New Delhi,
Dk.Biteko amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini India, Anisa
Mbega na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mafuta na Gesi India,
Sandeep Jain.
Wiki ya Nishati India itakutanisha Mawaziri na Watendaji Wakuu wa
Sekta ya Nishati kutoka maeneo mbalimbali duniani, watunga sera na
wavumbuzi wa teknolojia mbalimbali za kisasa za nishati kwa lengo la
kuja na mustakabali endelevu wa upatikanaji nishati.
Aidha, Wiki hiyo itahusisha pia maonesho ya teknolojia mbalimbali za
matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia
Katika ziara hiyo, Dk.Biteko ameambatana na baadhi ya Wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na baadhi ya
Watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake wakiongozwa na Kamishna
wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga.