NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Tutuba amependa ushirikiano unaofanywa baina ya Kampuni Airpay Tanzania na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) katika kuwafanya wananchi kurejesha mikopo ya bila riba inayotolewa na Serikali ya Zanzibar.
Ushirika huo wa ZEEA na Airpay ambayo ni Kampuni yenye lengo la kurahisisha mifumo ya malipo ya kifedha kidijitali kwa watu wa kawaida Wafanyabiasha na wajasiriamali wadogo wadogo inaelezwa kuwa utasaidia wakopaji kurejesha na kukopa fedha kwa wakati.
Gavana Tutuba ameyasema hayo leo Januari 32,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha BoT, ZEEA, Airpay pamoja na wadau mbalimbali kutoka Taasisi za kibenki na mitandao ya simu.
Alisema amefurahi kuona ZEEA wanashirikiana na Airpay katika kuleta mfumo wa kidijitali ili kusaidia namna nzuri ya kuwafanya wakopaji kurejesha fedha zinazotolewa na serikali bila riba ili ziweze kusaidia wananchi wengine na kwamba imani yake mfumo huo utasaidia urejeshwaji wa pesa hizo.
“Kwa Zanzibar kuna benki tatu PBZ, CRDB na TCB , hii mikopo wananchi wengi huko visiwani wanaipata kupitia ZEEA na kuna wadau mbalimbali wakiwemo Airpay na kampuni za huduma za simu kwa Zanzibar na hata Bara wanaosaidia kuhakikisha fedha hizi zinarejeshwa,”amesema.
Tutuba amesema watu wengi wanashindwa kurejesha lakini kwa namna ambavyo Airpay wametengeneza itarahisisha kila mtu huko aliko kurejesha mikopo hiyo hivyo kupunguza muda, usumbufu na hata nauli kwenda benki hivyo sehemu ya nauli kusaidia kurejesha mkopo.
“Serikali au benki inapokukuposha hasa fedha hizi ambazo hazina riba ni kuwasaidia wananchi wajiinue kiuchumi na kuanzia huku mtu anaweka rekodi nzuri hata ya kukopesheka katika mikopo mikubwa zaidi,”
“Hizo fedha sio zawadi ni uwezeshaji kiuchumi ili wajijengee faida na tunaendelea kuweka mifumo mizuri kusaidia urejeshwaji wa mikopo hiyo bila usumbufu na kila anayepata pesa hizo ajitahidi kujua serikali imewasaidia kujikwamua hivyo warejeshe,” amesema Tutuba
Aidha Tutuba amesema kwa upande wa ZEEA mikopo asilimia 28 ya mikopo Chechefu wengi wamelipa lakini wachache sababu zao za kutokulipa hazina mashiko hata kidogo.
“Ndio maana ZEEA na mabenki ya waliowakopesha yawafuatilie kila mmoja kwani wastani wa mikopo chechefu ilikuwa asilimia 3.3 kuishia Desemba mwaka jana tuko chini hivyo wafuatiliwe hawa nao ili waingizwe kwenye mifumo ili asipolipa asikopesheke tena milele sehemu yeyote ile,”amesema Gavana.
Naye Mihayo Wilmore kiongozi upande wa Mifumo kutoka Airpay Tanzania amesema kitu wanachotaka kukifanya ni kuweza kuhakikisha mteja hapati usumbufu katika urejeshaji.
“Mtumiaji anaweza kwenda kwa wakala yoyote kulipa bila usumbufu wowote changamoto ni mkopo unaochukuliwa na kushindwa kurejeshwa unakuwa mkopo chechefu sasa tumekuja kuomba Benki Kuu ya Tanzania ituruhusu kuchukua asilimia 33 ya kile ambacho kipo kwenye simu ya mteja ili aweze kurejesha kidogo kidogo kama ulikuwa na Sh. 10,000 tutachukua sh 3,000 kukupunguzia deni lako la Sh. 100,000,”amesema.
Amesema wanataka kutengeneza njia mbadala ili waweze kurejesha kidogo kidogo na kwamba kwa mujibu wa sheria ya BOT hivyo vitu vyote vinafanyika kabla na kuwa na makubaliano hasa kwa wale ambao wanashindwa kutoa ushirikiano wakitafutwa kulipa.
Kuhusu elimu kwa wananchi Mhiayo alisema ni zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa wamezungumza na wananchi na hata viongozi wa Serikali za mitaa.
“Haya maombi tunayaomba ili taratibu za kurejesha pesa kwenye mifumo ubadilike mfano umesafiri uko nje ya nchi ukajisahau mambo ya mfumo yatafanya kazi na ndio maana tumeomba BOT watupe nafasi ya kufanya hivyo,”ameeleza
Juma Burhan Mohamed Mkurugenzi Mtendaji ZEEA amesema, wao kama wakala wa uwezeshaji wananchi kiuchumi washatoa mikopo yenye thamani ya sh Bilioni 34.9 ambao umewafikia wanawake 14,000 na wanaume 9,000.
“Utoaji unakwenda vizuri kuanzia 2022 hadi 2024 lakini hili la mtandaoni ni jambo zuri maana mambo yako huko kwa sasa tumeona kuna haja ya kukaa pamoja na kuweza kuona sisi kama wakala kwa kushirikiana na taasisi nyingine tunawezaje kulifanya suala hili la kimtandao,”
“Wananchi wanapaswa kujua unapopewa fedha ya serikali sio yangu mimi bali ni ya watanzania , naamini kikao hiki leo kitatusaidia hata wao ambao walikuwa hawataki kurejesha watasaidiwa na mfumo kuweza kulipa,” amesema Juma ma kuongeza
“Chukua mkopo kwa manufaa yako rejesha ili Taifa liendelee hii ndio kauli mbiu yetu Zanzibar ili kiwanyanyua wananchi kiuchumi hivyo kila aliyenyanyuliwa kiuchumi arejesha kwa wakati na kujua namna marais wetu Hussein Ally Mwinyi na Samia Suluhu Hassan wanavyowapenda wananchi wao,”amehitimisha