*WB,
AfDB wampongeza Rais Samia kuwa kinara sekta ya nishati
NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MKUTANO wa Nishati wa Wakuu wa nchi za Afrika (Mission 300) uliofanyika Januari 27 na 28, 2025 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) umeelezwa kuwa umefungua mwanga na matumaini katika bara la Afrika kufikiwa na umeme wa uhakika.
Tanzania ilikuwa Mwenyeji wa mkutano huo uliohudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Burundi, Botswana, Congo, Comoros, Djibouti, Ethiopia, Gabon, Ghana, Guinea Bissau, Kenya, Lesotho, Liberia, Libya, Madagascar, Malawi, Mauritania, Nigeria, Sierra Leone, Somalia na Zambia.
Mkutano huo ambao ulihudhuriwa pia na wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali, Wakuu wa Mashirika ya Fedha ya Kimataifa, Mashirika ya Kimataifa, Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia kwa lengo la kuongeza kasi ya usambazaji umeme barani Afrika ili kuwaunganisha watu milioni 300 na umeme katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Kupitia mkutano huo umefanikiwa kupata ahadi za ufadhili wa Dola za Marekani Bilioni 40 kutoka Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ajili ya kuwezesha usambazaji wa umeme barani Afrika. Aidha, jumla ya nchi za Afrika 12 zimeingia kwenye Mipango Mahsusi wa Kitaifa kuhusu Nishati.
Zakia Juma ni mkazi wa Dar es Salaam na mmoja wa watu waliofuatilia kwa karibuni mkutano huo anasema, kwa namna alivyowaona viongozi wa Afrika anadiriki kusema kuwa wana dhamira ya dhati kuhakikisha nchi zao zinakuwa na umeme wa uhakika.
Anasema ni ukweli ulio wazi kuwa kama nchi za Afrika zikiwa na umeme wa uhakika basi zinaweza kupata maendeleo makubwa zaidi ya yaliyopo sasa na kuchochoa ukuaji wa uchumi pamoja na ajira.
“Umeme ndo maendeleo, niwapongeze viongozi wa Afrika ambao kabla ya kuja kwa mkutano huu kulikuwa na wazo hilo ambalo naona limefanikiwa kwa ukubwa, matumaini yetu hasa sisi wa Tanzania kupitia mipango iliyowekwa katika mkutano huu tutapa umeme wa uhakika tena wenye gharama nafuu,” anasema Juma.
Naye Charles Marwa mwanafunzi chuo cha Ustawi wa Jamii na mkazi wa Dar es Salaam anasema, amefurahi Tanzania kuwa wenyeji wa mkutano huo na anamatumaini makubwa kuwa fedha zitakazotolewa kuhakikisha nishati ya umeme inapatikana zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Anasema nchi za Afrika kwa muda mrefu zinapambana kupata maendeleo hivyo uwepo wa umeme wa uhakika utarahisha upatikanaji wa maendeleo hayo na ajira hasa kwa vijana.
“Nimekuwa nikifuatilia mkutano huu na nimeona kama umeleta matumaini mapya kwa nchi za Afrika kufikiwa na nishati ya umeme, niwaombe viongozi wetu kushikamana ili kila mtanzania afikiwe na umeme,” anasema
Awali akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan alisema Tanzania ni moja ya nchi 12 zinazotekeleza mpango huo mahususi wa taifa kuhusu nishati ambao utaongeza kasi kuunganisha umeme nchini hadi kufikia asilimia 72 ifikapo 2030.
Anasema ili kufanikisha mpango huo ndani ya miaka mitano ijayo inahitaji uwekezaji wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 13 ambapo kati ya hizo dola bilioni tano zitapatikana kutoka sekta binafsi.
“Tumepanga kuongeza uzalishaji wa umeme kutokana na nishati mchanganyiko ambapo mpaka sasa Tanzania inauwezo wa kuzalisha megawati 3,431 ambapo asilimia 58 inatokana na vyanzo vya maji, asilimia 35 ni gesi asilia na asilimia 7 inatokana na vyanzo vingine.
“Hivyo tumelenga kuongeza megawati 2,463 za nishati kutokana na jua, gesi asilia, upepo na vyanzo vingine ifikapo 2030.Tanzania ni kiungo muhimu katika kuunganisha nchi nyingine za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika na nishati ya umeme, jambo linalowezesha biashara ya umeme kutoka Afrika Kusini hadi Cairo, Misri,” anasema Rais Samia
Anasisitiza kuwa Tanzania inayo nafasi ya kuuza umeme, hadi mwezi Novemba 2024 na kwamba mahitaji ya umeme nchini Tanzania ni megawati 1,888 wakati uzalishaji ukiwa megawati 3,431.
“Kupitia mkutano huu, tumepanga kufikisha umeme kwenye vitongoji vyote, baada ya kufanikiwa kusambaza umeme katika vijiji vyote vya Tanzania ambapo mwelekeo wetu wa sasa ni kuvifikia vitongoji 64,359 ambapo mpaka sasa mpango wetu umeshavifikia vitongoji 32,827 na kazi inaendelea ya kuvifikia vitongoji vilivyobaki,” anasema Rais Samia
Aidha anasema Tanzania ina mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya kupikia unaolenga kupandisha kiwango cha matumizi ya nishati safi ya kupikia kutoka asilimia 10 ya sasa hadi asilimia 80 ifikapo mwaka 2030, ambapo mpango mahususi uliozinduliwa katika mkutano huo utatusaidia kufikia lengo hilo.
Naye Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema kuwa serikali ya Tanzania imeuchukulia mkutano huo kama kichocheo cha sera yake ya Taifa ya Nishati inayolenga kuendeleza nishati endelevu, uhifadhi na ufanisi.
Anasema sera hiyo pia inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kisasa za nishati na kuongeza mchango wa nishati mbadala katika uzalishaji ili kuimarisha upatikanaji, uhakika na usalama wa nishati.
“Ifikapo mwisho wa mwaka huu 2025, uwezo wa Tanzania kuzalisha umeme utaongezeka hadi megawati 4,000. Habari njema ni kwamba nishati yetu hii inatokana na vyanzo safi na mbadala vinavyonufaisha wakazi wa vijijini na mijini, hata hivyo miundombinu ya umeme imefika katika vijiji vyote 12,318 nchini.
“Pamoja na maendeleo haya madogo yaliyofikiwa bado tunahitaji uwekezaji zaidi katika sekta ya nishati. Tuna matarajio ya kukuza shughuli za kiuchumi hasa katika sekta ya viwanda na madini jambo ambalo linahitaji uwekezaji wa kimkakati zaidi katika sekta ya nishati,” amesema Dk. Biteko
Anasema Rais Dk. Samia amekuwa mstari wa mbele katika kukuza upatikanaji wa suluhisho la nishati safi ya kupikia barani Afrika na kwamba jitihada hizo zimeungwa mkono na mkakati wa kitaifa na yamejumushwa katika azimio litakalotiwa Saini.
Amesema maazimio ya nishati ya kitaifa yaliyotayarishwa na nchi 12 zitakazokuwa za majaribio yatatoa mfumo wa utekelezaji wa hatua zilizoratibiwa ili kufungua uwekezaji zaidi kutoka kwa serikali, wabia wa maendeleo, mashirika ya misaada na sekta binafsi katika kufanikisha malengo ya upatikanaji wa nishati.
Kwa upande wake Rais wa Benki ya Dunia (WB), Ajay Banga amesema wanaweza kubadilisha sura ya Afrika kwa kuwa na juhudi za pamoja za kuunganisha rasilimali zilizopo kuhakikisha nishati ya umeme inawafikia wananchi wengi zaidi Afrika ifikapo 2030.
Naye Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk. Akinumwi Adesina anasema Benki ya Dunia (WB) na AfDB watatoa Dola za Marekani Bilioni 40 kama kianzio cha kufanikisha mpango wa kupeleka nishati ya umeme kwa wananchi barani Afrika.
Anasema Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa kwa kufanya vizuri katika uwekezaji wa miundombinu ya umeme kwa kuwafikishia nishati ya umeme wananchi katika vijijini vyote 12,318.
“Nawahakikishia kuwa lengo la kuwafikishia umeme watu milioni 300 Afrika linakwenda kufanikiwa, tunahitaji uwazi na uwajibikaji katika kufikisha lengo hili. Mkutano huu unalengo la kuifungua Afrika kwenye eneo la nishati ya umeme, kuhakikisha wananchi katika nchi za Afrika wanaunganishwa na umeme,” anasema Dk. Adesina
Mkutano huo ni juhudi za pamoja zinazoongozwa na Wakuu wa Nchi za Afrika kwa kushirikiana na benki ya AfDB, Benki ya Dunia (WB) na wadau wa maendeleo ili kukabiliana na changamoto ya nishati inayowakabili Waafrika milioni 600 ambao bado hawajafikiwa na umeme.