NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko amesema kuwa mpaka sasa vijiji vyote Tanzania vimefikiwa na umeme wa gridi ya taifa na kwamba hatua hiyo inawawezesha wananchi kuwa na uhakika wa nishati hiyo katika kuitumia kwenye shughuli zao za kimaendeleo.
Biteko ameyasema hayo Leo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika (Mission 300) unaofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.
Amesema Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Sekta ya Nishati nchini Tanzania kwani kipindi chake cha uongozi amewezesha nchi kuwa na uzalishaji wa umeme wa kutosha kwa ziada kubwa.
“Ni katika wakati wake ambapo kila kijiji nchini Tanzania kimefikiwa na umeme wa gridi ya taifa. Kwa juhudi zake Tanzania imeweza kuunganisha gridi yake ya umeme na nchi nne jirani,” amesema na kuongeza
“Rais Samia katika mawanda ya kimataifa amesukuma ajenda ya nishati safi ya kupikia na kuongoza majukwaa mbalimbali ya nishati ya kupikia duniani,” amesema Biteko
Hata hivyo amesema Rais Samia kuanzia siku ya kwanza, amefanya kazi bila kuchoka kuhakikisha kwamba nchi inakidhi mahitaji ya nishati na kutimiza matarajio ya watu wetu.