NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema kuwa serikali ya Tanzania inauchukulia Mkutano wa Nishati wa Nchi za Afrika kama kichocheo cha sera yake ya Taifa ya Nishati inayolenga kuendeleza nishati endelevu, uhifadhi na ufanisi.
Dk. Biteko ameyasema hayo leo Januari 27, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano huo unaofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC).
Amesema sera hiyo pia inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kisasa za nishati na kuongeza mchango wa nishati mbadala katika uzalishaji ili kuimarisha upatikanaji, uhakika na usalama wa nishati.
“Ifikapo mwisho wa mwaka huu 2025, uwezo wa Tanzania kuzalisha umeme utaongezeka hadi megawati 4,000. Habari njema ni kwamba nishati yetu hii inatokana na vyanzo safi na mbadala vinavyonufaisha wakazi wa vijijini na mijini, hata hivyo miundombinu ya umeme imefika katika vijiji vyote 12,318 nchini.
“Pamoja na maendeleo haya madogo yaliyofikiwa bado tunahitaji uwekezaji zaidi katika sekta ya nishati. Tuna matarajio ya kukuza shughuli za kiuchumi hasa katika sekta ya viwanda na madini jambo ambalo linahitaji uwekezaji wa kimkakati zaidi katika sekta ya nishati,” amesema Dk. Biteko
Amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amekuwa mstari wa mbele katika kukuza upatikanaji wa suluhisho la nishati safi ya barani Afrika na kwamba jitihada hizo zimeungwa mkono na mkakati wa kitaifa na yamejumushwa katika azimio litakalotiwa Saini.
Amesema maazimio ya nishati ya kitaifa yaliyotayarishwa na nchi 14 zitakazokuwa za majaribio yatatoa mfumo wa utekelezaji wa hatua zilizoratibiwa ili kufungua uwekezaji zaidi kutoka kwa serikali, wabia wa maendeleo, mashirika ya misaada na sekta binafsi katika kufanikisha malengo ya upatikanaji wa nishati.
Naye Rais wa Benki ya Dunia (WB), Ajay Banga amesema wanaweza kubadilisha sura ya Afrika kwa kuwa na juhudi za pamoja za kuunganisha rasilimali zilizopo kuhakikisha nishati ya umeme inawafikia wananchi wengi zaidi Afrika ifikapo 2030.
Kwa upande wake Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB0, Dk. Akinumwl Adesina amesema Tanzania imekua mfano wa kuigwa kwa kufanya vizuri katika uwekezaji wa miundombinu ya umeme kwa kuwafikishia nishati ya umeme wananchi katika vijijini vyote 12,318.
“Nawahakikishia kuwa lengo la kuwafikishia umeme watu milioni 300 Afrika linakwenda kufanikiwa, tunahitaji uwazi na uwajibikaji katika kufikisha lengo hili. Mkutano huu unalengo la kuifungua Afrika kwenye eneo la nishati ya umeme, kuhakikisha wananchi katika nchi za Afrika wanaunganishwa na umeme,” amesema
Waziri wa Fedha na Mipango, Zambia, Dk. Situmbeko Musokotwane amresema anawashukuru Watanzania kwa kuiuzia umeme Zambia kwa sababu wanakabiliwa na upungufu wa nishati hiyo ya umeme.
mwishoo