NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
JESHI la Polisi kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema kufuatia mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika unaotarajiwa kufanyika Januari 27 na 28 mwaka huu, barabara tisa zitafungwa huku bodaboda na bajaji hazitaruhusiwa kuingia mjini kwa kipindi hicho cha mkutano.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa kanda Maalum hiyo ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amezitaja barabara hizo ambazo zitakazofugwa kwa muda kupisha misafara ya viongozi ni barabara ya Nyerere kutokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwenda katikati ya Jiji.
Muliro amesema barabara nyingine ni ya Sokoine, Kivukoni na Lithuli kuanzia taa za Gerezani
kwenda Hoteli ya Johari Rotana, Hyatt Regency hadi Ikulu.
Barabara nyingine ni ya Ohio kutokea Kivukoni kwenda Hoteli ya Serena, barabara ya Ghana kutokea barabara ya Ohio kwenda Hoteli ya Onomo, Barabara ya Bibi Titi kutokea makutano ya barabara za Ohio na Ally Hassan Mwinyi kwenda Hoteli ya Crowne.
Amesema Barabara ya Azikiwe kwenda Hoteli ya Four Points, Hoteli ya Golden Tulip City Center na Hoteli ya Holiday Inn, Barabara ya Morogoro kutokea Sokoine kwenda Hoteli ya Tiffany, Barabara ya Makunganya kutokea Azikiwe kwenda Hoteli ya Tiffany pamoja na Barabara ya Garden kutokea barabara ya Lithuli kwenda Hoteli ya
Southern Sun pamoja na Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa JNICC.
Amesema katika kipindi chote cha Mkutano huu watumiaji wengine wa barabara mnashauriwa kutumia barabara za Uhuru, Kawawa kupitia Magomeni, Kigogo kuelekea Temeke, barabara ya Morogoro na Msimbazi, Morogoro na Lumumba na kwa wale wanaotokea maeneo ya Chanika wanashauriwa kutumia njia mbadala ya mradi ya SGR ili waje kutokea barabara ya Mandela
na Uhuru.
“Aidha kwa sababu za kiusalama wale wanaotumia vyombo vya moto kama pikipiki za magurudumu mawili (bodaboda) na magurudumu matatu (bajaji) vyombo hivyo havitaruhusiwa kuingia katikati ya Jiji kwa muda ambao umetajwa wakati wageni hao wakiwa bado wapo.
Bodaboda na bajaji wameshauriwa na kuelekezwa kuishia maeneo kweKwa barabara ya Ally Hassani Mwinyi wataishia daraja la Salender.
Kwa barabara ya Morogoro wataishia Jangwani, Kwa barabara ya Kawawa kutokea Magomeni wataishia Kigogo
sambusa, Kwa barabara ya Uhuru kutokea Buguruni wataishia Ilala Boma, kwa barabara ya Nyerere kutokea Airport na Veta wataishia taa za Veta, Kwa barabara ya Kilwa wataishia Mivinjeni.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam linatoa wito kwa wananchi
kufuata utaratibu huu na Jeshi la Polisi litajitahidi kuzisimamia hizo njia mbadala ili kupunguza msongamano kwa kadri itakavyowezekana.