NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
IMEELEZWA kuwa kuwa Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo Afrika (AFDB) zinawajibika kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kusaidia nchi za Afrika kuharakisha Mpango wake wa kupeleka nishati ya umeme kwa Waafrika milioni 300 ifikapo 2030 ( Mission 300)
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam jana na Makamu wa Rais wa Benki ya AFDB anayeshughulikia Nishati, Kevin Kariuki wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika unaotarajiwa kufanyika hapa nchini Januari 27 hadi 28 mwaka huu.
Mkutano huo unabeba ajenda tano ikiwemo ushirikishwaji wa sekta binafsi katika kuvutia mitaji ya Uwekezaji katika sekta ya nishati, pamoja na kuwezesha uunganishaji wa umeme kwa gharama nafuu.
Kariuki amesema licha ya benki hizo kutoa fedha pia ni muhimu kwa viongozi wa Afrika kuhakikisha rasilimali fedha zitakazopatikana zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
”Uaminifu katika suala hili ni wa muhimu sana kwa maana fedha zinatolewa hivyo kama serikali hazitajidhatiti katika kusimamia hatutaweza kupata matokeo chanya, lengo lazima tulitimize na litafanikiwa kwa uwezo wa Mungu na viongozi wetu wa Afrika,” amesema Kariuki
Aidha Makamu huyo ametoa rai kwa nchi za Afrika kuweka kipaombele cha kutenga sehemu ya rasilimali fedha za mapato yake ya ndani ili kuongeza kasi ya kufikisha umeme kwa haraka zaidi kwa wananchi.
Mkutano wa nishati wa Wakuu wa nchi barani Afrika utafanyika hapa nchini ambapo zaidi ya wakuu wa nchi 25 kutoka Barani Afrika , wakiwemo mawaziri wa fedha na nishati wa Afrika pamoja na wadau wa maendeleo wa mashirika ya kimataifa watashiriki katika mkutano huo.