NA ATUPAKISYE MWAISAKA, DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe amewapongeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa kuandaa na kuratibu Mkutano wa pili ambao umewaleta pamoja wadau ili kujadiliana mafanikio na changamoto zinazoikabili sekta hii ya biashara hususani katika eneo la Sajili na Leseni za Biashara ambapo BRELA ndiyo lango la uanzishaji wa biashara nchini.
Aidha Kigahe amesema Mtu au Taasisi yeyote haiwezi kuanzisha biashara bila kuwa imesajiliwa na BRELA au imepata Leseni ya Biashara kwa zile biashara za Kundi “A”.
Kauli hiyo imetolewa leo Oktoba 25,2024 katika Mkutano wa pili wa Wadau wa Brela uliofanyika jijini Dar es salaam
Pia, Kigahe amewapongeze wadau wote wa BRELA (Taasisi za Serikali, Sekta Binafsi, Wawekezaji, Wafanyabiashara, Taasisi za Fedha, Wajasiriamali, Vyombo mbalimbali vya habari) kwa kutenga Murda wao adimu na kushiriki katika mkutano huu ambao ni muhimu sana katika uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara nchini.
“Nafahamu kila mmoja aliyefika mahali hapa ameacha shughuli zingine muhimu na kuja kushiriki nasi katika mkutano huu. Nimefarijika sana kwa mashirikiano haya kati ya Serikali na Sekta Binafsi.
“Ushiriki wenu katika Mkutano huu ni ishara kuwa juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Jemedari wetu Mkuu, Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mpendwa Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassan za kuweka mazingira bora, wezeshi na shirikishi ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini. Ukuaji wa biashara na uchumi nchini unaendelea kuimarika na kuweza kufikia malengo ya Serikali katika Mpango wa Maendeleo wa Tanzania wa kufikia uchumi wa kati na endelevu ifikapo mwaka 2025.” amesema Kigahe
Amesema,Katika kipindi hiki, tangu BRELA walipoandaa Mkutano wa kwanza na sasa, naamini kuwa kuna maboresho mengi yamefanywa na BRELA kama Wakala ya Serikali chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ili kuongeza ufanisi na ubora wa huduma zake. Nitoe rai kwa Taasisi zingine za Serikali ambazo hazina utaratibu huu, kuweza kuiga mfano huu mzuri ili kuweza kujipima kwa kupata maoni na mtazamo kutoka kwa wadau badala ya kujifungia na kujitathmini wenyewe maofisini.
Aidha, Kigahe amesema ,BRELA haiwezi kufanikiwa katika kutekeleza majukumu yake ikiwa peke yake, inategema ushirikiano na ukaribu na Sekta za Umma na Sekta Binafsi. Ndiyo maana Mkutano huu ni muhimu sana kufanyika ili kufanya tathmini ya wapi BRELA imetoka, ilipo sasa na wapi inaelekea ukizingatia nafasi yake katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa.
“Nii matarajio yangu kuwa Mkutano huu ni nyenzo muhimu katika kuifanya BRELA kuwa taasisi bora na ya mfano katika kutoa huduma bora za sajili na leseni, kutoa elimu kwa jamii ya wafanyabiashara na wawekezaji ili uwekezaji na biashara zinazofanyika ziwe na tija, faida zipatikane kwa wafanyabiashara na Serikali ikusanye kodi kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo na uchumi wa nchi uweze kukua na kuimarika.
” Aidha, Mkutano huu uwe chachu kwenu washiriki na muweze kusambaza elimu kwa Wananchi ambao hawajapata fursa ya kuwepo mahali hapa kwani uelewa wao utapunguza kero mbalimbali na gharama za urasimishaji biashara zitapungua na hatimaye mazingira ya biashara nchini kuwa bora na wezeshi.”amesisitiza Naibu Waziri huyo
Katika hatua nyingine Kigahe ameonesha kuvutiwa na Kauli Mbiu ya Mkutano wa Mwaka huu ‘Mifumo ya Kitaasisi inayosomana na Uwezeshaji wa Biashara nchini’ (Interoperability of Institutional Systems and Business Facilitation).
Akizungumzia juu ya Kauli Mbiu hiyo,Kigahe amesema inalenga kuleta mjadala mpana wa Mifumo ya Kitaasisi kusomana kwa lengo la kutoa huduma zote kwa njia ya mifumo. Mtakumbuka kuwa Serikali ilishatoa maelekezo kwamba ifikapo Mwezi Desemba, 2024, Taasisi za Serikali ziwe na mifumo inayosoamana. Maelekezo haya pia, yalizingatia kuondoa usumbufu na kero zisizo za msingi kwa Sekta Binafsi kwa kuombwa nyaraka hizo hizo kwenye Taasisi mbalimbali za Serikali, wakati nyaraka hizi zingeweza kupatikana kwa njia za mifumo.
“Nafahamu kwamba kuanzia mwaka 2018 BRELA imekuwa ikitoa huduma zake za Sajili na Leseni kwa njia ya mtandao kupitia mifumo ya Usajili kwa njia ya Mtandao (Online Registration System) na Dirisha la Taifa la Biashara (Tanzania National Business Portal). Mifumo hii imepunguza muda, gharama na bughudha kwa Wawekezaji na Wafanyabiashara ambao walikuwa wanasafiri umbali mrefu kufika katika Ofisi za BRELA Dar es Salaam kwa ajili ya kupata huduma hizo.
“Utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao umerahisisha mambo ambapo wafanyabiashara wanaweza kuomba kusajili au kupata Leseni za Biashara zao wakiwa maofisini kwao na wakapata cheti cha Usajili au Leseni pale pale alipo bila kuhitaji kufika katika ofisi za BRELA.
“Serikali ilifarijika sana na Taarifa ya Maboresho ya Mazingira ya Biashara na Uwekezaji iliyotolewa na Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji katika mkutano wa Uzinduzi wa Taarifa hiyo tarehe 11 Septemba, 2024 katika ukumbi huu huu wa Mlimani City. Katika taarifa hiyo ilielezwa kwamba moja ya mafanikio ya maboresho hayo ni pamoja na BRELA kuweza kusajili Makampuni na Majina ya Biashara pamoja na kutoa Leseni za Biashara ndani ya siku moja. Hii ni hatua kubwa katika uboreshaji wa mazingira ya Biashara na imetokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara na Taasisi zake katika kuboresha mazingira ya Biashara na Uwekezaji.” ametanabaisha Kigahe
Pamoja na mambo mengine Kigahe alitoa rai kwa kuwa taka Brela wasibweteke na maboresho hayo ya kimfumo kwani Teknolojia inabadilika kila siku, hivyo muweke mkakati wa kuhakikisha mnakwenda sambamba na maboresho ya Kiteknolojia ili huduma yenu izidi kuwa bora na wezeshi.
“Nimetaarifiwa kwamba Viongozi na Maafisa kutoka nchi mbalimbali wamekuwa wakifika BRELA kwa ajili ya kujifunza namna ya utoaji wa huduma kwa ufasaha na kwa njia ya mifumo. Mmepata ugeni kutoka nchi za Burundi, Sudan Kusini na Kenya ambao wote wametoka katika nchi jirani na ni za ukanda huu wa Afrika Mashariki. Hii inaonyesha kufanikiwa kwa kiwango kikubwa kwa Dira ya BRELA iliyoainishwa katika Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2021/22-2025/26) ya kuwa kituo cha mfano katika Ukanda kwa utoaji wa huduma za Sajili na Leseni za biashara (To be a Centre of Excellence in the Region for Business Registrations and Licensing Services)
“Pamoja na mafanikio hayo, kama nchi bado tunayo fursa ya kuboresha zaidi, na katika hili nimetaarifiwa kwamba BRELA wanafanya maboresho ya mifumo yake ya Usajili na Utoaji wa Leseni ili kuondoa changamoto zilizobainika katika mifumo iliyopo sasa na kuja na mfumo mpya ambao utaongeza kasi, ufanisi na usalama wa taarifa za sajili, leseni na wawekezaji nchini. Ni matarajio yangu na Serikali kwa ujumla kwamba maboresho hayo, yatapunguza zaidi muda na masaa ya sajili na leseni kuwa ndani ya masaa machache, kuongeza kasi ya urasimishaji wa biashara na kuongeza idadi ya wawekezaji na wafanyabiashara na hivyo kuongeza wigo wa ajira na walipa kodi.”amejinasibu Kigahe.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela ,Godfrey Nyaisa ameishukuru Wizara ya Viwanda na Biashara hasa watumishi, wakiongozwa na Katibu Mkuu Dk.Hashil Abadallah kwa ushirikiano na miongozo ambayo wamekuwa wakiwapa, ushirikiano huo umetuwezesha kutimiza majukumu yetu kwa ufanisi na kwa weledi, lengo likiwa ni kuhakikisha BRELA tunatoa huduma bora na kwa wakati.
Nyaisa amesema,Wizara ya Viwanda na Biashara imekuwa kiungo muhimu sana kwetu kwa kusaidia na kuhakikisha BRELA inakuwa na mifumo na nyaraka mbalimbali za kiutendaji kazi.
“Kwa namna ya kipekee kabisa naomba kutambua uwepo wa Taasisi dada kutoka upande wa Zanzibar; Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali (BPRA) wanaotoa huduma sawa na BRELA, na Ofisi ya Hakimiliki Zanzibar (COSOZA) wanaotoa huduma sawa na COSOTA. Tumekuwa tukishirikiana nao kwenye utendaji kazi kwa karibu sana kwenye maeneo mbalimbali Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.
” ikumbukwe kuwa Oktoba 27, 2023, BRELA tuliandaa Maonesho na Mkutano wa Wadau kwa lengo la kujadili mafaniko, fursa na changamoto zinazohusu sajili mbalimbali zinazotolewa na BRELA, pamoja na urasimishaji wa biashara kiujumla. Urasimishaji wa biashara ni mchakato kwa maana ya “process”. Usajili aidha wa Kampuni au Jina la Biashara ni sehemu ya mchakato tu wa Urasimishaji wa biashara. Mara baada ya kusajili Mfanyabiashara anatakiwa kupata leseni au vibali kutoka Mamlaka nyingine za Serikali ikiwa ni pamoja na Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN), Leseni ya Biashara na Vibali kutoka Mamlaka za Uthibiti “Regulatory Authorities”. Uwepo wa Taasisi za Umma na Binafsi kwenye Mkutano huu wa pili wa BRELA na wadau wake utasaidia kujadili mafanikio, fursa na changamoto za Sekta ya Biashara.”ameeleza Nyaisa
Amesema kuwa Mkutano huu wa Pili wa BRELA na wadau wake una washiriki kutoka Sekta za Umma kwa maana ya Wizara mbalimbali, Taasisi na Mashirika ya Umma. Pia, kuna ushiriki wa Sekta Binafsi zenye mashirikisho yenye wanachama wengi, Wawekezaji, Wamiliki wa Viwanda, Wafanyabiashara, Wajasiriamali, Wabunifu, Ofisi za Mawakili na wafanyabiashara wadogo kabisa. Mchanganyiko huu wa washiriki kutoka Sekta za Umma na Sekta Binafsi utaleta majadiliano yenye tija kwa manufaa ya pande zote mbili.
“Utakumbuka kwenye Mkutano wa mwaka jana, Wizara yako ilitoa maelekezo mahususi kwa BRELA, kuwa Mkutano huu uwe ni mkutano utakaokuwa unafanyika kila mwaka na BRELA iandae majibu na mpango wa utekelezaji wa maoni, ushauri na mapendekezo ya wadau. Maelekezo haya yalipokelewa na kufanyiwa kazi, ndiyo maana leo tunashiriki Mkutano huu wa Pili wa BRELA na Wadau wake. Pia, Mheshimiwa Mgeni Rasmi, mimi pamoja na watumishi wenzangu tutatoa majawabu ya utekelezaji wa maoni, ushauri na mapendekezo ya wadau ya mwaka jana. Kwa kufanya hivi, ni moja ya kigezo kinachotoa taswira ya BRELA kuchukulia maoni ya wadau kwa uzito mkubwa, na pia hii ni sehemu ya uwajibikaji wa moja kwa moja kwa wadau wetu.
” Kauli Mbiu ya Mkutano wa Mwaka huu ni “Mifumo ya Kitaasisi inayosomana na Uwezeshaji wa Biashara nchini” (Interoperability of Institutional Systems and Business Facilitation). Wote ni mashaidi kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mama yetu Mpendwa Samia Suluhu Hassan, amekuwa akitoa maelekezo na miongozo ya Mifumo ya Taasisi za Serikali kusomana. Lengo ni kurahisisha utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao na kuondoa usumbufu usio wa lazima kwa wananchi ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara kwa ujumla.
“Washiriki wengi wanaijua historia ndefu ya BRELA toka ikiwa Idara ndani ya Wizara ya Viwanda na Biashara, ikijulikana kama “Ofisi ya Msajili wa Makampuni” mbali na kuwa ilikuwa ikitoa huduma za sajili zikiwa ni pamoja na Majina ya Biashara “Business Names”, Alama za Biashara na Huduma “Trade and Service Marks, Hataza “Patents” na utoaji wa Leseni za Viwanda “Industrial Licenses”.
“Mageuzi makubwa yalianza kufanyika Desemba 3, 1999, baada ya BRELA kuwa Wakala wa Serikali chini ya Sheria ya Wakala za Serikali “Executive Agency Act No. 30 of 1997”. Mabadiliko haya yalilenga kuharakisha utoaji huduma na kuboresha mazingira ya utendaji kazi. Wengi wenu ni mashahidi kuwa bado mabadiliko hayo hayakukidhi kiu zenu. Mifano midogo tu, usajili wa kampuni ulitoka miezi mitatu m wiki mbili, upatikanaji wa majalada bado ulikuwa changamoto kubwa, mazingira ya ofisi yalikuwa na mchanganyiko na ofisi nyingine binafsi, lakini pia vishoka walitumia fursa hii kufanya ulaghai na wengine kujifanya kuwa ni watumishi wa BRELA.”, amefafanua Ofisa Mtendaji Mkuu huyo.
Mbali ya hayo Nyaisa amesema kuwa mwaka 2015 BRELA ilianzisha mfumo wa kwanza wa usajili wa Majina ya Biashara kwa njia ya Mtandao “Online Business Name Registration System – OBRS”. Mfumo huu ulitengenezwa na watumishi wa BRELA kwa kushirikiana na vijana wengine wakitanzania, hiki ni kiashiria tosha kuwa vijana wetu wakiwezeshwa wanaweza.
” Januari 4,2018, BRELA ilianza kutumia mfumo mpya wa Usajili kwa Njia ya Mtandao “Online Registration System- ORS”, mfumo huu unatoa huduma zote za sajili na za baada ya sajili “Registration and Post Registration” zikiwa ni pamoja na sajili za Makampuni, Majina ya Biashara, Alama za Biashara na Huduma, Hataza pamoja na Leseni za Viwanda. Kwa upande wa Leseni za Biashara za Kundi “A” zilizohamishiwa BRELA kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara pia zinatolewa kwa njia ya Mtandao kupitia Mfumo wa “Tanzania National Business Portal – TNBP”. Huduma hizi zimerahisisha sana wateja kupata huduma popote pale walipo, huduma nyingine zikiwa ni kwa siku moja tu. Kabla ya mifumo hii kuanza wateja walikuwa wanalazimika kutoka sehemu zote za nchi kuja kupata huduma Dar es Salaam. Huduma nyingine zilikuwa zinagharimu kiasi cha Sh.1,000 lakini wateja walilazimika kutoka Mbeya, Arusha, Mwanza, Rukwa na mikoa mengine kufuata huduma hii.
“Mfumo huu wa ORS umetimiza miaka sita sasa, ni dhairi teknolojia na baadhi ya sheria zimebadilika sana. Hivyo, sisi kama BRELA tulishaanza maboresho ya Mfumo huo kwa kuufanya uwe bora na rafiki zaidi. Nikiri kuwa katika mfumo wa sasa kuna baadhi ya taarifa zinazolazimu kujazwa zaidi ya mara moja, kitu ambacho mfumo ungeweza kuvuta taarifa hizo bila kuhitaji kujazwa tena. Zoezi la maboresho lilishirikisha maoni ya wadau kwani wao ndiyo watumiaji wakubwa wa Mfumo huu. Nitumie fursa hii, kuwashukuru sana wadau wetu kwani wamekuwa mstari wa mbele kutoa maoni na michango pale tunapohitaji kutoka kwao, siyo kwenye mifumo tu hata kwenye maboresho ya sheria sita tunazozisimamia na BRELA. Pindi, Mfumo utakapokamilika tutawaita tena wadau wetu na kuwapitisha katika maeneo yote muhimu yaliyoboreshwa.
” Maboresho haya yamezingatia uwepo wa huduma zingine, mfano upande wa Leseni za Biashara, BRELA inaendelea na mashauriano na mamlaka zingine ili kutumia mfumo mmoja wa Leseni za Biashara utakao kuwa na uwezo wa kutoa Leseni za Kundi “A” zinazotolewa na BRELA na Leseni za Kundi “B” zinazotolewa na Serikali za Mitaa “Local Government Authorities” bila kuathiri mapato ya Halmashauri husika. Kwa namna ya kipekee kabisa Mheshimiwa Mgeni Rasmi naishukuru sana Wizara yako kwa kusimamia kwa dhati majadiliano ya kuwa na mfumo mmoja wa utoaji Leseni za Biashara. Uanzishwaji wa mfumo huu mmoja wa Leseni utaisaidia sana Serikali kwenye takwimu pamoja na kuthibiti upotevu wa mapato kwa kuondoa leseni za kuandikwa kwa mikono.ameongeza Nyaisa
Ameendelea kusema kuwa Agosti, 2021, BRELA iliboresha mazingira ya ofisi zetu kwa kuhamia ofisi mpya zilizopo Mtaa wa Shaaban Robert na Samora Avenue. Ofisi hizi mpya zina mazingira bora ya utendaji kazi, tofauti na Ofisi za zamani ambapo kulikuwa na mwingiliano mkubwa na ofisi nyingine binafsi, hivyo kutoa mwanya kwa “vishoka” kujifanya sehemu ya watumishi wa BRELA, hivyo kutapeli baadhi ya wafanyabiashara au kuwalipisha gharama za juu zisizo na uhalisia.
“Maboresho ya Sheria mbalimbali za BRELA yanaendelea kwani sheria za sasa ni za muda mrefu mbali na kufanyiwa marekebisho mbalimbali, mfano Sheria ya Leseni za Biashara ni ya mwaka 1967, Sheria ya Hataza ni ya mwaka 1987, Sheria ya Alama za Biashara na Huduma ni ya mwaka 1986, Sheria ya Makampuni ni ya Mwaka 2002. BRELA inafanya maboresho ya sheria hizi ili kuendana na mifumo, teknolojia, utendaji kazi na mazingira ya sasa. Zoezi hili linaratibiwa vizuri na Wizara yako kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Pia, kwa upande wa watumishi tunaishukuru sana Serikali kwa kutupa watumishi wa kutosha na wenye weledi, BRELA itaendelea kuajiri kulingana na uhitaji wa watumishi.
BRELA kama Ofisi ya Taifa ya Miliki Ubunifu inaendelea na uratibu wa zoezi la kuandaa Sera ya Taifa ya Miliki Ubunifu inayoandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na wadau. Sera hii itaongeza wigo wa sajili na ulinzi mpya za Miliki Ubunifu. Pia, BRELA inaendelea na mipango yake kabambe ya utoaji wa elimu kwa umma, ili kuhakikisha huduma za Mtandao zinatumika nchini kote. Kwenye eneo la bunifu, nguvu nyingi imewekwa kwenye kutoa elimu kwa Vyuo Vikuu na Taasisi za Ufundi, kwani bunifu nyingi zinaanzia huko. Ndani ya miaka miwili, maombi ya Hataza “Patents” yameongezeka kwa zaidi ya asilimia mia moja “amehitimisha Nyaisa