NA ASHRACK MIRAJI,SAME, KILIMANJARO
MKUU wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amefungua milango ya maendeleo ya utalii kwa kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Nkoba Mabula, leo Septemba 25, 2024.
Katika mkutano huo, Mgeni alisisitiza kwamba utalii si tu fursa ya kiuchumi, bali pia njia ya kuboresha maisha ya wananchi na kuhifadhi mazingira, huku akielezea jitihada za kutangaza vivutio vya wilaya ili kuvutia wawekezaji na kuimarisha uchumi wa eneo hilo.
“Hapa Same tumezungukwa na hifadhi mbalimbali na kutambua umuhimu wa uhifadhi, mwaka huu tulifanya tamasha kubwa la Same Utalii Festival. Tamasha hili liliwakutanisha wadau mbalimbali, na wananchi wameweza kuona umuhimu wa kuhifadhi mazingira na wanyamapori,” alisema Mgeni.
Aliongeza kuwa tamasha hilo lilikuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha jamii kuhusu faida za uhifadhi na jinsi unavyoweza kuchangia katika ustawi wa kiuchumi.
Mgeni alitoa shukrani kwa Rais kwa kuendelea kutekeleza sera za maendeleo ya utalii, akieleza kuwa Wilaya ya Same ina vivutio vingi ambavyo havijatangazwa.
Aidha, alizungumzia tamasha lililopangwa kufanyika mwezi Desemba, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano na Wizara katika kutangaza tukio hilo ili kuvutia wawekezaji.
“Tumeona ongezeko la wageni, na kampuni tano tayari zimejitokeza kusafirisha watalii baada ya kuona muitikio wa watu kwenye tamasha la mwaka jana,” aliongeza, akionesha matumaini makubwa kuhusu maendeleo ya utalii katika wilaya hiyo.
Mgeni alimalizia kwa kutoa wito kwa Wizara kuendelea kuunga mkono juhudi za wilaya katika kukuza utalii, akiamini kwamba hatua hizo zitachangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya wananchi na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Naibu Katibu Mkuu, Mabula, alisisitiza umuhimu wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo wilayani humo.
“Nimekuja kuona baadhi ya vivutio vyetu. Nchi hii imebarikiwa, lakini tunahitaji orodha ya vivutio ili tuweze kufanya kazi zaidi,” alisema.
Mabula alitaja umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na wananchi katika matumizi ya rasilimali za misitu, mashamba, na hifadhi ili kuongeza mapato.
Aidha, aliupongeza uongozi wa wilaya kwa kufanikisha tamasha la utalii, lakini alisisitiza umuhimu wa kuwa na vituo vya taarifa za utalii kila wilaya. “Takwimu sahihi zitasaidia katika kutenga bajeti na kuhakikisha uwekezaji unafanyika katika maeneo yenye faida,” alifafanua.
“Utalii ni fursa, lakini hadithi nzuri zitakazotufanya tuuze vivutio vyetu ni muhimu. Kaeni na wazawa mtambue vivutio vyote, wawape hadithi, na muwawezeshe wawe waongoza watalii,” alisisitiza Mabula.
Aliongeza kuwa, Wizara iko tayari kutoa ushirikiano kufanikisha tamasha hilo, akiamini litakuwa fursa ya kuimarisha utamaduni wa Wapare na kuwahamasisha wawekezaji kuzingatia mila na desturi za eneo. “Tunataka fedha zinazopatikana kutokana na utalii zibaki hapa Same,” alisisitiza.