NA JANETH JOVIN
RAIS Samia Suluhu Hassan amevitaka vyama vya siasa kuheshimu falsafa ya 4R (Maridhiano, Uvumilivu, Haki na Uwajibikaji) na kwamba 4R hizo si sababu ya utovu wa nidhamu na kukiuka sheria za nchi.
Rais Samia ameyasema hayo leo Septemba 17,2024 wakati akifungua mkutano Mkuu wa maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi kwa mwaka 2024 na maadhimisho ya miaka 60 ya jeshi hilo yaliyofanyika katika viwanja vya Jeshi la Polisi (CCP) Kilimanjaro.
Amesema 4R si sababu ya utovu wa nidhamu na watu kukiuka sheria za nchi na kusisitiza sheria zipo palepale na kwamba wanasiasa wasisahau mapito waliyopitia.
Serikali imejitahidi sana kurejesha Uhuru wa vyama vya siasa, Uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa raia, kwa ujumla wale waliokuwa uhamishoni walirejea nchini, waliokuwa na kesi za jina na wengine tulizifumbia macho, waliokuwa jela tuliwatoa sasa wapo huru na wanaendelea na shughuli zao ikiwemo za kisiasa lengo letu likiwa kuwaleta watu pamoja ili tuweze kujenga nchi,” amesema Rais Samia
Amesema watu hao wanaposahau yote hayo na kutoa kauli zinazoharibu au kuwarudisha nyuma wao hawatakuwa tayari kuruhusu hayo yatokee na kusisitiza kuwa amani ya nchi atailinda kwa gharama yeyote ile.