*Asema vikao vyote vya kupanga maovu atavipata
*Aapa serikali yake itailinda,kuitetea Katiba
*Aahidi kuimarisha ulinzi,usalama na uhai wa kila Mtanzania
*Watakaoharibu amani ya nchi kuchukuliwa hatua
*Ataka kila mtu atimize wajibu wake kipindi cha uchaguzi
NA JANETH JOVIN
RAIS wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan amesema vikao vyote vitakavyo kwenda kupanga uovu wataupata na kusisitiza kuwa Serikali yake imeapa kuilinda na kuitetea Katiba ya Tanzania na kwamba watafanya kila linalowezekana kuimarisha ulinzi wa maisha na uhai wa watanzania kwa kuwa ni jukumu lao.
Rais Samia ameyasema hayo leo Septemba 17, 2024 wakati akifungua mkutano mkuu wa maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi kwa mwaka 2024 na maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Polisi Tanzania katika Viwanja vya jeshi hilo (CCP) Kilimanjaro.
“Nataka kuwaambia vikao vyote vitakavyokwenda kupanga uovu tutaupata, mmepanga kushusha moto mpaka Samia aseme basi naondoka, hiyo ni serikali au serikali ya samaki, maana samaki kila akiwa mkubwa na akili inafanyaje….., Serikali hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haiondoshwi hivyo.
“Sasa kwa kutumia kofia ya Amiri Jeshi Mkuu niseme kwamba tumeapa kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba tutafanya kila linalowezekana kuimarisha ulinzi wa maisha na uhai wa watanzania kwa kuwa ni jukumu letu,” amesema Rais Samia
Wakati huo huo,Rais Samia amelitaka Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wale wote watakaojaribu kuhatarisha amani ya nchi kwa kisingizio cha uchaguzi.
“Nalitaka Jeshi la Polisi kuwa macho katika kipindi chote cha kabla, wakati na baada ya uchaguzi, polisi hakikisheni yeyote anayejaribu kuhatarisha amani ya nchi yetu kwa kisingizio za chaguzi hizo anachukuliwa hatua haraka na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” amesema Rais Samia
Amesema katika kipindi cha uchaguzi kila mmoja anatakiwa kujipanga kufanya kazi vizuri zaidi kwa kuhakikisha taifa la Tanzania linabaki kuwa moja na salama.
“Uchaguzi utapita lakini Tanzania irabaki, tunataka kubaki na Tanzania iliyo salama na yenye utulivu ili shughuli za maendeleo ziweze kuendelea,” amesema Rais Samia