*Asisitiza ushuru wa huduma kutatua changamoto za wananchi
NA MWANDISHI WETU,MTWARA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ameelekeza Watanzania kunufaika na rasilimali zinazochimbwa katika maeneo yao kwa kutoa fursa mbalimbali ikiwemo ajira.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk.Doto Biteko leo Septemba 10, 2024 mkoani Mtwara katika hafla ya kukabidhi leseni ya uendelezaji wa eneo la ugunduzi wa gesi asilia katika Kitalu cha Ruvuma, eneo la Ntorya ambapo Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) pamoja na Kampuni za ARA Petroleum Limited na Ndovu Resources Ltd ni wabia.
“ Mhe. Rais alielekeza wananchi waliopo maeneo yenye rasilimali wanufaike kabla ya maeneo mengine, alitoa kibali cha mradi mkubwa wa gesi na tutajenga kiwanda cha kuzalisha gesi na kuboresha kituo za kuzalisha umeme Songa.” amesema Dk.Biteko.
Ameongeza katika mradi wa Ntorya vitachimbwa visima namba 1 na 2 pamoja na kujenga bomba la kusafirisha gesi kutoka katika kisima hadi Madimba kilomita 34 na katika kipindi cha miezi sita bomba litakuwa limejengwa.
Aidha, Dk.Biteko ameielekeza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusimamia utekelezaji wa miradi katika halmashauri kupitia ushuru unaotokana na huduma.
“ Tunakusanya ushuru wa huduma lakini hatutengi fedha, wakurugenzi wa halmashauri kaeni kwenye mabaraza toeni sehemu ya ushuru wa huduma na kuipeleka kwa wananchi miradi inapofanyika mfano mwaka 2023 TPDC walitoa shilingi milioni 164 na nwaka huu wametoa shilingi milioni 198. Tupeleke fedha kidogo kwa watu kwa kuwa kuna fedha inapatokana kidogo kidogo TAMISEMI simamieni jambo hili ili tusipate malalamiko kutoka kwa wananchi, amesema Dk.Biteko.
Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amesema kuwa juhudi za Serikali za kuongeza upatikanaji wa nishati ya gesi asilia nchini zinakwenda sambamba na kuwaunganishia umeme wananchi wa maeneo ambayo gesi inatoka (Madimba, Msimbati na Songo Songo).
Kwa upande wa Madimba jumla ya vitongoji 18 na Msimbati jumla ya vitongoji 13 ambavyo havina umeme vitakuwa vimeunganishiwa umeme ifaikapo mwezi Desemba, 2024. Aidha, kwa upande wa Songo Songo vitongoji vyote vitakuwa vimeunganishiwa umeme ifikapa tarehe 31 Oktoba, 2024. Vilevile, Serikali kupitia REA inaendelea na kazi ya kupeleka umeme katika vijiji 30 vya Mkoa wa Lindi ambapo kazi hiyo itakamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2024.
Aidha, katika kuhakikisha kuwa hali ya upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara inaendelea kuimarika, mnamo tarehe 31 Machi, 2024 Serikali ilikamilisha kufunga mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa MW 20 ha hivyo kuondoa tatizo la upungufu wa umeme katika mikoa hiyo. Vilevile, mradi wa Gridi Imara wa kuunganisha Mtwara na Lindi kupitia Tunduru upo katika hatua ya utekelezaji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalum, George Mkuchika amesema kuwa awali wabunge wa Mkoa wa Mtwara na Lindi walimweleza Dkt. Biteko changamoto ya nishati katika mikoa hiyo na hasa Madimba eneo iliyopo gesi na sasa wanaipongeza Serikali kwa kuanza mradi huo wa Ntorya.
Aidha, Mkuchika ameshukuru kwa kuanza utekelezaji wa maagizo ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kuhusu ujenzi wa kituo cha afya Madimba na taa za barabarani na ni imani yao kuwa miradi hiyo itakamilika kwa wakati.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Kilumbe Ng’enda amesema kuwa matumizi ya gesi yamepungua kwa kuwa na ongezeko la umeme katika Gridi ya Taifa na gesi iliyokuwa inatumika kwa ajili ya umeme kwa sasa itaelekezwa maeneo mengine ambapo zaidi ya asilimia 60 ya umeme uliokuwa inazalishwa ilitokana na gesi.
“ Utoaji wa leseni katika mradi huu ni hatua kubwa kitalu hiki kitazalisha futi za ujazo trilioni 1.6 hili ni jambo kubwa tunakupongeza wewe na Rais samia. Tunaridhishwa na kazi kubwa inayoendelea hasa katika sekta ya gesi na baada ya mchango wake mkubwa katika umeme sasa ikatoe mchango mkubwa katika nishati safi ya kupikia na uendeshaji mitambo na magarii ili kusaidia nchi kuelelekea katika matumizi ya nishati safi.” amesema Ng’enda.
Balozi wa Omani nchini Mhe. Saud bin Hilal Alshaidani amesema kuwa tukio kukabidhi leseni ya kuendeleza kitalu hicho linaunganisha nchi za Tanzania na Oman na kuwa na itasaidia uchumi wa Tanzania.
“ Tunatarajia katika ushirikiano huu tutapata faida na kusaidia jamii ya Mtwara pamoja na kuitambulisha Tanzania huko duniani kama wazalishaji wa gesi,” ameeleza Balozi huyo.
Mbunge wa Mtwara Vijijini, Shamsia Mtamba amempongeza Rais Samia kwa kukubali kutekeleza mradi huo wa uendelezaji na ugunduzi wa gesi Ntorya Kata ya Nanguruwe kwa kuwa italeta tija na chachu ya maendeleo na kukuza uchumi wa watu wa Mtwara na nchi kwa jumla.
“ Tunaona mambo mbalimbali yameanza kufanyika kwa kuwa na rasilimali ya gesi kwa mfano maelekezo yako ya Kijiji cha Msimbati yameanza kutekelezwa na ombi langu kwako mradi huu ukianza kufanyakazi wananchi wa eneo hili wapate ajira ili kujiendeleza kiuchumi.”
Mhe. Mtamba ameongeza kuwa licha ya kuwa yeye ni Mbunge wa Chama Cha Wananchi (CUF), Dk.Biteko na Serikali kwa ujumla imekuwa ikitekeleza maombi yake kuhusu miradi ya maendeleo ya jimbo lake.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa safari ya nchi kuelekea ugunduzi wa gesi asilia imeanza muda mrefu ambapo mwaka 2010 ugunduzi mkubwa ulifanyika katika kina kirefu cha bahari pamoja na nchi kavu kiasi cha futi 57.54.
Mhandisi Mramba ametaja baadhi ya faida ya ugunduzi wa gesi hiyo ni kuwa ni kuimarika kwa usalama wa nishati, kuongeza uzalishaji umeme na kuwa na mchanganyiko mzuri zaidi wa nishati zinazipatikana nchini.
Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Musa Makame amesema kuwa mradi huo ulianza kwa kushirikiana kati ya Serikali, TPDC na Kampuni ya Ndovu Resources.
“ Mwaka 2017 uchimbaji ulifanyika na kupata gesi, hadi sasa tuna futi trilioni 1.6 ambazo zimegundulika na kuhakikiwa, na mwaka huu hadi ujao tunachimba kisima na tayari tuna visima viwili na tunaenda kuchimba cha tatu,” amesema Makame.
Amefafanua kuwa TPDC inajenga bomba la kusafirisha gesi na kiwanda kidogo cha kuchata gesi iwe kimiminika na kupeleka kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa na mabomba na kisha kwenda kwenye maeneo mengine.
Aidha, Shirika hilo litatoa fedha kiasi cha Sh Milioni 750 kwa ajili ya
kujenga kituo cha afya ikiwa ni sehemu ya faida ya uwepo wa mradi huo.