NA DANSON KAIJAGE,DODOMA
UONGOZI wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, umewapiga msasa Waandishi wa Habari wa Jiji la Dodoma kwa kuwapatia masomo juu ya umuhimu wa afya ya akili.
Akifungua mafunzo ya siku moja Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili, Dk.Paul Lawala amesema Waandishi wa Habari wana kila jukumu sahihi la kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa afya ya akili na kuifanya jamii kuachana na unyanyapaa kwa watu wanaoonekana kuwa na changamoto ya afya ya akili,ambapo kauli mbiu ni “Afya ya Akili…. Ni Afya
Afya ya Akili…. Inaanza na mimi
Hakuna Afya bila Afya ya Akili”.
“Tunapokutana hapa leo, tunafanya hivyo tukiwa na lengo moja kuu, kuboresha uelewa na ujuzi wa waandishi wa habari kuhusu masuala ya afya ya akili kupitia mawasilisho yatakayofuatiwa na mijadala , ili kuoanisha afya ya akili na utoaji taarifa sahihi kwa jamii kupitia vyombo vya Habari.
“Waandishi wa habari mna nafasi ya kipekee na ya muhimu katika jamii. Kupitia kazi zenu, mnatoa habari, elimu, na burudani, na kwa kufanya hivyo, mnaathiri kwa hasi au chanya jinsi watu wanavyofikiria, wanavyotenda, na wanavyojihusisha na masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na afya ya akili.
“Kwa hivyo, tunapokutana hapa leo, ni muhimu kutambua kuwa Vyombo vya Habari vina nafasi muhimu sana katika kuelimisha umma kuhusu afya ya akili na kupunguza unyanyapaa unaohusishwa na afya ,changamoto na magonjwa ya akili” ameeleza Dk.Lawala.
Amesema ni kwa Nini Mafunzo ya afya ni muhimu ameeleza kuwa ,Afya ya akili ni sehemu muhimu ya afya ya jumla ya mtu binafsi na jamii kwa kuwa Afya ya Akili ni Afya,Afya akili inamhusu kila mtu na hakuna afya bila afya ya akili.
Hata hivyo amesema mara nyingi, imekuwa ikipuuzwa au kutofahamika vizuri.
“Hali hii imechangia kuwepo kwa unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya wale wanaopambana na changamaoto za Afya ya Akili na magonjwa ya akili.
“Kwa upande mwingine, Waandishi wa Habari wanaweza kusaidia kubadilisha hali hii kwa kutoa taarifa sahihi, zinazoelimisha, na zenye uwiano uliotafitiwa kuhusu afya ya akili. Hapa ndipo umuhimu wa mafunzo haya yanapokuja.
“Lengo la mafunzo haya ni kuwapa ninyi, waandishi wa habari, maarifa na ujuzi unaohitajika ili kuripoti kwa usahihi na kwa uwajibikaji kuhusu afya ya akili.
” Tunataka kuhakikisha kwamba mnakuwa na uwezo wa kutambua habari sahihi, kuzuia kusambaza habari zilizopotoshwa, na zaidi ya yote, kuweza kutoa taarifa kwa njia ambayo inaondoa unyanyapaa na kuongeza uelewa katika jamii.”ameeleza.
Katika ufunguzi huo wa mafunzo Dk.Lawala amesema kuwa Mada Muhimu Zitakazojadiliwa na
Mafunzo hayo yatajikita katika mada kadhaa muhimu, ikiwa ni pamoja na,
Self-understanding,Kuelewa jinsi ya kujitambua na kusimamia afya zetu za akili.
Mada nyingine amezitaja kuwa ni jinsi ya kuripoti kuhusu afya ya akili kwa kuzingatia mitazamo ya kihistoria na ya kisasa, kutoka katika muktadha wa Afrika na dunia kwa ujumla.
Ameendelea kuzitaja mada ni kuangalia jinsi Viongozi wa kidini na kisiasa wanavyoweza kuathiri jamii kuhusu masuala ya afya ya akili, na nafasi ya vyombo vya habari katika kuboresha athari hizi.
“Mada hizi ni muhimu katika kuhakikisha kuwa ripoti zenu zinakuwa na uwiano, unaozingatia maadili, na zinasaidia katika kujenga jamii yenye afya bora ya akili.”amefafanua zaidi Dk.Lawala.
Akihitimisha hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo hayo amesema kuwa Waandishi wa Habari, wana jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa wanajenga jamii ambayo inatambua na kuthamini afya ya akili.
“Waandishi wa Habari, mna nafasi ya pekee. Ninaamini kwamba kupitia mawasilisho na mijadala tutakayofanya, mtapata maarifa na ujuzi wa kutosha ambao utawasaidia kutekeleza majukumu yenu kwa uwajibikaji na kwa manufaa ya jamii yetu”ameeleza Mkurugenzi huyo.