NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa wito kwa serikali kuridhia mkataba wa kimataifa wa Ulinzi kwa Watu dhidi ya Kupotea na Kutekwa wa mwaka 1994, ili kukabiliana na ongezeko la matukio ya kupotea na kutekwa kwa baadhi ya watu.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam leo Agosti 30,2024 na Mkurugenzi Mtendaji LHRC, Anna Henga wakati akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari juu ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wahanga wa matukio ya kutoweka na kutekwa.
Henga amesema mkataba huo unaweka mfumo madhubuti wa kushughulikia ukiukwaji matukio ya utekaji katika Jumuiya ya Umoja wa Mataifa ikiwemo Tanzania hata hivyo amesema bado Tanzania haijaridhia mkataba huo ili kuufanya uwe sehemu ya sheria zake.
Amesema kufuatia ongezeko la matukio ya utekaji nchini ni sababu tosha ya kuifanya Tanzania kuridhia mkataba huo ili kuweka ulinzi thabiti kwa wananchi wake dhidi ya matukio hayo.
“Tunatoa wito kwa serikali kuridhia mkataba huu kwa kuwa umeweka taratibu madhubuti za ulinzi wa watu dhidi ya matukioya utekaji, hatua hii sio tu itaonesha kujidhatiti katika Jumuiya ya Umoja wa Kimataifa kudhibiti vitendo hivyo bali pia itaongeza imani kwa wananchi wake juu ya ulinzi na usalama wao,” amesema Henga
Amesema ibara ya kwanza ya mkataba huo inabainisha na kuweka katazo la watu kuwekwa vizuizini na kutekwa kwa kuwa inakwenda kinyume na ulinzi wa haki za binadamu.
“Ibara ya pili inatafsiri vitendo vya kutoweka na utekaji ikijumuisha vitendo vya kukamatwa. kuwekwa kizuizini, kutekwa au namna yeyote ya kumnyima mtu uhuru iwe kwa kufanywa na serikali, vyombo vyake au kwa maelekezo ya serikali kwa kuelekeza chombo au mtu huyo kuficha taarifa za alipo mtu aliyekamatwa au kutekwa.
“Na ibara ya tatu na sita ya mkataba huo, inataka mamlaka kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki na kuwafikisha watu wote waliyohusika na matukio hayo ya kuficha taarifa za mtu aliyetekwa katika vyombo vya kisheria,” amesema
Aidha amesema wanatoa wito kwa serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama ifanye uchunguzi wa kina wa malalamiko dhidi ya matukio hayo hususani katika kipindi cha hivi karibuni kwa kuwa vitendo hivyo vinaathiri zaidi watoto, wanawake na jamii kwa ujumla.
Amesema serikali inapaswa kuimarisha mifumo a ulinzi na usalama katika ngazi ya jamiikwa kushirikiana na wananchi ili kudhibiti matukio hayo.