NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema bado kuna fursa nyingi hapa nchini ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje.
Ametoa kauli hiyo jana usiku (Jumatano, Agosti 21, 2024) wakati akizungumza na mamia ya Wadau na Washiriki waliohudhuria tukio la USIKU WA UTALII ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za Tamasha la Kizimkazi 2024 lililofanyika kwenye uwanja wa Maendeleo ya Sheria wa Dimbani, Kizimkazi, Zanzibar.
Amesema kwa kutumia fursa za utamaduni, wanyama na utalii wa fukwe Tanzania inaweza kuongeza idadi ya watalii kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na hali ilivyo sasa. “Hapa Kizimkazi tuna samaki aina ya pomboo ambaye ana sifa zote za kuingia kwenye utalii. Tuendelee kuimarisha utalii wa fukwe na tuwatumie pomboo kuchochea utalii kama ambavyo wenzetu wa Cuba wanawatumia.”
“Cuba ni nchi ndogo lakini inapokea watalii wengi sana. Wanao walimu wa kuwafundisha samaki hawa kucheza na binadamu, wanafundishwa kucheza muziki. Na sisi Tanznaia tunao pomboo wa kutosha. Ni kwa nini na sisi tusiige kutoka kwa wenzetu? Tufanye hili ili tuweze kuongeza fursa za utalii.”
“Bado tunazo fursa nyingi zaidi ya hizi, lakini hatujamudu kusheneneza soko letu kwa kutumia utalii wa ndani. Na sisi tunadhani utalii ni watu wa nje tu, hapana. Lakini utalii wa ndani ni eneo jingine linaloweza kuongeza idadi ya watalii nchini,” amesema.
Ili kuendelea kulikuza tamasha hilo, Waziri Mkuu amewataka Makatibu Wakuu wa wizara zinazohusika na masuala ya utamaduni kwa pande zote mbili wahakikishe wanaunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni muasisi wa tamasha hilo pamoja na Kamati ya maandalizi ili idadi ya washiriki na wageni kutoka nje iweze kuongezeka.
“Matangazo na promosheni vianze miezi sita kabla ya tamasha ili watu waandae bajeti zao mapema na kwa njia hiyo tutaongeza hamasa ya ushiriki wa tamasha hili. Wizara na taasisi husika tumieni mitandao ya kijamii, tovuti, na vyombo vya habari ili kuongeza hamasa.”