NA DANSON KAIJAGE, DODOMA
LICHA ya ya utekelezaji wa Kanuni za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini za mwaka 2023 (CSR) bado utekelezaji wa Kanuni hizo umelalamikiwa na Wadau wakidai kwamba utekelezaji wake umekuwa ni mgumu kwenye baadhi ya maeneo hususani yanapo patikana madini.
Kutokana na kuwepo kwa mvutano huo wamiliki wa Migodi walilazimika kuwasilisha maombi kwa Waziri wa Madini ili Kanuni hizo zifanyiwe maboresho kwenye maeneo ambayo yanaleta ugumu kuyatekeleza.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini Dk.Steven Kiruswa wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau kuhusu Marekebisho ya Kanuni za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini kwa jamii (CSR)za mwaka 2023 kilichofanyika jijini Dodoma.
Akizungumza na Wadau,Wabunge,Wenyeviti wa Halmashauri na Wakuu wa Wilaya Dk.Kiruswa amesema kuwa lengo kuu la kikao hicho ni kupata fursa ya kutoa maoni kuhusu maboresho ya Kanuni za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini kwa Jamii, (CSR) za mwaka 2023.
Amesema kuwa mwaka 2023 Wizara ya Madini ilitunga Kanuni za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini kwa lengo la kutoa mwongozo kwenye fedha inayotolewa na Kampuni za Madini kwa Jamii inayozunguka migodi kama sehemu ya wajibu wa kampuni hizo kwa jamii kupitia miradi inayotekelezwa kupitia programu za CSR.
Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa lengo jingine la Kanuni hizo ni kuhakikisha kuwa kunakuwepo na ushirikishwaji wa pamoja kati ya Jamii na kampuni za madini katika utekelezaji wa miradi ya jamii.
Hata hivyo amesema kuwa licha ya kanuni za wajibu wa Wamiliki wa Leseni za madini za mwaka 2023 kuendelea kutekeleza bado zimeibua malalamiko makubwa na mvutano mkali kati ya Wamiliki wa migodi na halmashauri hususani halmashauri zenye madini mengi.
Hadi sasa Kanuni za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini za mwaka 2023 zinaendelea kutekelezwa kwa malengo yaliyotajwa.
“Hata hivyo, utekelezaji wa kanuni hizo umelalamikiwa na wadau wakidai kwamba umekuwa ni mgumu kwenye baadhi ya maeneo na hivyo kuwasilisha maombi kwa Waziri wa Madini ili Kanuni hizo zifanyiwe maboresho kwenye maeneo ambayo yanaleta ugumu kuyatekeleza.
” Malalamiko hayo yaliwasilishwa kwa Waziri wa Madini wakati wa majumuisho ya Bajeti ya Wizara ya Madini katika Bunge la Bajeti la Mwaka wa fedha 2024/2025.
“Baada ya kupokea malalamiko hayo Waziri wa Madini aliahidi kuitisha kikao cha Wadau mapema iwezekanavyo ili kuweza kupata maoni yatakayosaidia kufanya maboresho kwenye Kanuni hizo.”ameeleza Dk.Kiruswa.
Sambamba na hilo Dk.Kiruswa amesema kuwa tangu Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ilipofanyiwa maboresho Mwaka 2017 na kuwekewa Kifungu cha 105 ambacho kinaelezea utaratibu mzima wa kuandaa na kutekeleza suala la Wajibu wa Kampuni kwa Jamii, suala hilo limekuwa na mafanikio ukilinganisha na kipindi cha nyuma ambapo Kampuni zilikuwa zikiwajibika kwa jamii kwa utaratibu waliojiwekea wenyewe.
Amesema kuwa kipindi cha mwaka 2018 hadi 2023, zaidi ya Sh.Billioni 96.6 za kitanzania zimetumika katika kutekeleza miradi mbalimbali ya CSR na Wamiliki wa Leseni za Madini katika Halmashauri zenye uchimbaji wa Madini nchini.
Kwa upande wake Rais wa wamiliki wa migodi Mikubwa na yakati
John Bina amesema kuwa yeye kama Rais wa wamiliki wa migodi simamo wake ni kuhakikisha wamiliki wa migodi wanasimamia wenyewe miradi ambayo wamepanga kuitekeleza badala ya kutoa pesa katika halmashauri.
Hata hivyo amesema kuwa kumekuwepo na mvutano wa kutaka halmashauri kuchukua asilimia 60 na sehemu yanapopatikana madini kuchukua asilimia 40 jambo ambalo amesema sio sahihi.
“Tunataka sehemu ambapo yanapatikana madini wachukue asilimia 60 na Halmashauri ichukue asilimia 40 kwa kuwa ina vyanzo vingi vya mapato.
“Pia ni vyema yanapopatikana madini watu wawe na uchumi imara na wawe na fedha mifukoni siyo watu wanakuwa masikini au uchumi dhaifu na ni vyema kuwashirikisha wananchi miradi wanayoitaka”amesema Bina.
Naye Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu akizungumza muda mfupi baada ya ufunguzi wa kikao hicho amesema ni vyema fedha za wamiliki wa migodi ambazo utoa kama gawio zikaelekezwa katika Halmashauri ili waweze kuzisimamia kama wanavyosimamia fedha za miradi kutoka serikalini.
Jambo jingine amesema kuwa miradi mingi inachelewa kutokana na fedha za SCR kuchelewa na kusababisha kutofikia malengo kwa wakati.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wachimbaji Madini Martha Kayaga amesema pamoja na kutoa fedha za maendeleo kutoka kwa wachimbaji lakini kanuni bado zina changamoto kubwa ambazo zinasababisha mvutano kati ya wamiliki wa migodi na Halmashauri.