

NA PHILIPO HASSAN,ARUSHA
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Utalii, Nkoba Mabula amewasihi wageni wanaoshiriki kongamano la A 109 – Universala Kongreso De Esperanto” jijini Arusha kutembelea vivutio vya Utalii vilivyopo nchini Tanzania ambavyo ni pamoja na Mlima mrefu zaidi unaosimama peke yake duniani, Mlima Kiliamjaro, Hifadhi ya Taifa Serengeti pamoja na Zanzibar.
Mabula aliyasema hayo wakati alipokuwa akishiriki chakula cha jioni na jumuiya ya wazungumzaji na wapenzi wa lugha ya kiesperanto katika hafla iliyofanyika tarehe 05.08.2024 katika ukumbi wa mikutano ya kimataifa wa AICC Jijini Arusha .
Aidha, Mabula alisema “Ndugu wageni wetu tunawakaribisha sana Tanzania hivyo kwa wale ambao bado hamjapata fursa ya kwenda kutalii basi baada ya kongamano hili nendeni mkatalii Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro na Serengeti ambapo ni takribani saa moja kwa ndege kutokea Arusha pamoja na visiwa vya Zanzibar”
Kongamano hilo linalofanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika katika nchi ya Tanzania lina lengo la kuwakutanisha na kuwaunganisha wazungumzaji na wapenzi wa lugha ya kiesperanto ulimwenguni kote ambapo limewakutanisha wajumbe zaidi ya 800 kutoka mataifa zaidi ya 65 duniani na litafanyika kwa takribani siku saba (03/08/2024 hadi 10/08/2024)
Mabula aliambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Dk.Thereza Mugobi pamoja na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Jully Lyimo kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania.( TANAPA)