NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WATU 558 wa Wilaya ya Ilala na vitongoji vyake wamefanyiwa uchunguzi na wengine kupewa matibabu ya magonjwa ya moyo katika kambi maalumu ya Mhe. D. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba.
Kambi hiyo maalumu ya siku nne iliyomalizika jana imefanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika Zahanati ya Bungoni Wilaya ya Ilala kwa kushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa jimbo la Ilala Mussa Azzan Zungu.
Akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Eva Wakuganda alisema asilimia 67 ya watu wote waliofanyiwa vipimo vya moyo wamekutwa na magonjwa mbalimbali ya moyo ikiwemo shinikizo la juu la damu, moyo kutanuka, moyo kushindwa kufanya kazi na kuziba kwa mishipa ya damu.
“Katika kambi hii pia tumeweza kuwafanyia uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa watoto 75 ambapo kati yao watoto 12 tuliwagundua kuwa na matatizo ya matundu kwenye moyo”, alisema Dk. Wakuganda
Alisema katika kambi hiyo watu 215 walipewa rufaa kufika JKCI kwaajili ya kuendelea na matibabu zaidi na wale waliohitaji kutumia dawa walipewa dawa bila gharama.
“Sambamba na upimaji wa magonjwa ya moyo katika kambi hii watu 400 wamepimwa kipimo cha homa ya ini na kupewa chanjo hiyo bila gharama”, alisema
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Bungoni Dk. Ester Akili alimshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilala Mussa Azzan Zungu kwa kuwafikishia huduma za kibingwa za matibabu ya moyo wananchi wa Ilala bila gharama.
Alisema mwitikio wa watu kujitokeza kupima moyo umekuwa mkubwa tofauti na walivyotarajia kwani watu kutoka Wilaya ya Ilala na wilaya za jirani waliweza kujitokeza kufanya uchunguzi wa afya.
Tunaishukuru sana JKCI kwa kutuletea wataalamu hawa mabingwa wa moyo, kupitia kambi hii watu wameweza kukitafuta kituo chetu mahali kilipo na kufika kwani kituo hiki ni kipya na watu wengi walikuwa hawakifahamu.
“Zahanati ya Bungoni ni mypa tangu ianze kutoa huduma ina miezi saba sasa, tunashukuru kupitia kambi hii zahanati yetu imetambulika katika jamii ya watu kutoka maeneo mbalimbali”, alisema
Naye mwananchi aliyepatiwa huduma katika kambi hiyo William Kiwazo alisema alikutwa na shida ya moyo miaka mitano iliyopita lakini baada ya kupata matibabu na kuendelea vizuri hakuweza kurudi tena hospitali kuangalia maendeleo yake.
Kiwazo alisema kushindwa kwake kuendelea kufuatilia matibabu kumetokana na bima yake ya afya kuisha muda wake miaka miwili iliyopita na kushindwa kukata bima nyingine.
“Nilifanyiwa uchunguzi JKCI miaka mitano iliyopita na kukutwa na tatizo la moyo ambalo nilipewa dawa lakini baada ya hapo sijarudi tena hospitali kutokana na kadi yangu ya bima kuisha muda wake na kushindwa kukata bima nyingine”, alisema Kiwazo
Kiwazo alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kupima afya zao pale fursa za upimaji wa magonjwa mbalimbali zinapojitokeza kupunguza gharama ya kuzifuata mahali zilipo.