NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
VIONGOZI mbalimbali wa Serikali wamepongeza huduma za matibabu na elimu ya lishe zinazotolewa katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) lililopo katika maonesho ya 48 ya kimataifa ya biashara Dar es Salaam.
Pongezi hizo zimetolewa leo wakati viongozi hao walipotembelea banda la JKCI na kusema JKCI imeonesha mabadiliko makubwa katika kutoa huduma kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Akizungumza alipotembelea banda hilo Waziri wa Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui alisema JKCI kutumia huduma ya afya mtandao kuweka miadi ya kuonana na daktari ni moja ya teknolojia ya kisasa inayomsaidia mgonjwa kupata huduma za afya kwa wakati.
“Matumizi ya teknolojia katika Taasisi hii yanatumika vizuri sana kwani mfumo wa huduma za afya mtandao unaotumika kwa wananchi kukutana na wataalamu wa JKCI kupitia mtandao unatuwezesha kuzungumza na daktari tukiwa mahali popote duniani”, alisema Mazrui
Kwa upande wake Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Tanzania Awadhi Haji aliwapongeza wataalamu wa JKCI kwa kutoa huduma kwa wananchi katika maonesho ya Sabasaba.
Kamishna Haji alisema wananchi wanaposogezewa huduma karibu uwapa nafasi kutumia muda huo kupima afya tofauti na kama wangeambiwa waifuate huduma hiyo mahali zilipo hospitali.
“Nimetembelea banda hili na kupata elimu nzuri sana kuhusu magonjwa ya moyo, wananchi wanaopenda kupata elimu sahihi kuhusu magonjwa haya wasisite kutembelea banda la JKCI”, alisema Kamishna Haji
Naye Naibu Waziri wa Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Hassan Hafidh aliupongeza uongozi wa JKCI kwa kuwa mstari wa mbele kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo nchini.
Hafidh alisema kutoa huduma za moyo katika maonesho ya Sabasaba kunawapa fursa wananchi wengi kupima afya zao kwani maonesho hayo yanatembelewa na wananchi wengi.