NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WANANCHI wa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani wajitokeza kupima moyo katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) lililopo katika maonesho ya 48 ya kimataifa ya biashara Dar es Salaam.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliotembelea banda la JKCI wamewapongeza wataalamu wa JKCI kwa kuwafikishia wananchi huduma za matibabu pamoja na elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa hayo.
Lameck Kalulu amesema JKCI imekuwa na ubunifu mkubwa katika kutoa huduma za matibabu ya moyo kwani wamekuwa wakiongeza ujuzi na kuifanya taasisi hiyo kukidhi viwango vya kimataifa.
“Kupitia ubunifu wa Taasisi hii hapa sabasaba tumekutana na huduma ya matibabu majumbani, huduma hii inawasaidia sana wagonjwa na kuwapunguzia safari za kwenda hospitali mara kwa mara”, amesema Kalulu.
Amesema huduma nyingine aliyoikuta katika banda hilo ni huduma ya afya mtandao ambayo inampa nafasi mwananchi kuwasiliana na daktari kupata ushauri wa afya popote alipo bila ya kufika Hospitali.
“Leo nikihitaji huduma ya kumuona daktari wa JKCI sina haja kufunga safari kuifuata hospitali mahali ilipo nitaingia kwenye mfumo wao wa kuonana na mtaalamu mtandaoni nitaonana na daktari na pale itakapohitajika ndio nitaenda hospitali”, amesema Maluku
Rehema Ally mkazi wa Temeke amesema alipita katika banda la JKCI kuangalia vilivyopo ndani lakini kutokana na huduma nzuri zinazotolewa naye akavutiwa kufanya vipimo vya moyo kuangalia afya yake.
“Nimefurahia huduma zinazotolewa katika banda la JKCI, nimepokelewa vizuri na kushauriwa kufanya vipimo vya kuchunguza afya yangu na baada ya hapo nimepata elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo”, amesema Ally
Naye mkazi wa Dar es Salaam Godfrey Mosha amesema serikali ilipowekeza katika Taasisi ya Moyo haikuwekeza pabaya kwani taasisi hiyo imekuwa msaada kwa wananchi hasa wananchi wa hali ya chini.
“Mfano sahihi wa Taasisi hii ni uhalisia wa huduma wanazozitoa hapa sabasaba kwani huduma hizi zimelenga kuwafikia watu wenye hali zote kuweza kupima afya zao”, ameeleza Mosha
Amesema wananchi waliokuwa na matamanio ya kupima moyo wasisite kufika katika maonesho ya 48 ya kimatiaifa ya biashara Dar es Salaam katika banda la JKCI kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.