NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
RAIS wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa mauzo ya nje ya bidhaa zetu nchini yalipanda kutoka Sh. Trilioni 12.3 mwaka 2019 hadi kufikia Sh. Trilioni 17.3 sawa na Dola za Marekani Bilioni 6.56 mwaka jana.
Rais Samia ameyasema hayo leo Julai 3,2024 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba yaliyofunguliwa rasmi na Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi
Amesema serikali itaendelea kujenga, kuboresha na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo ya miundombinu ili kuhakikisha wanaongeza tija kwa uzalishaji kwa wingi na sifa.
“Tutakamilisha miradi ya miundombinu ili bidhaa zinazozalishwa ziweze kufika kwa urahisi kwenye masoko yaliyokusudiwa,” amesema Rais Samia
Aidha Rais Samia amesema Maonesho hayo ya Sabasaba kwa mwaka huu yamezikutanisha zaidi ya kampuni 3486 ya ndani nan je ya nchi na kwamba hiyo inaonesha ukuaji na mvuto wa jambo hilo.
“Mvuto huu umechangiwa na juhudi za serikali katika kusimamia misingi imara na thabiti kwenye kujenga uchumi jumuishi na shindani kiwenye nyanja mbalimbali ikiwemo biashara, viwanda na uwekezaji.
“Ni ukweli usiopingika njia moja wapo ya kufikia azma hii ni uendelezaji na uimarishaji wa ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa na hivyo kufungia fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji,” amesema Rais Samia
Hata hivyo amewataka wafanyabiashara kutumia maenesho hayo kukuza biashara zao na kuzitumia taasisi za serikali kufanikisha azma hiyo ya kufanya biashara kwenye nchi za nje hasa eneo huru la biashara Afrika (AfCFTA).
“Wafanyabishara kutoka Tanzania kupitia maonesho haya jifunzeni kutoka kwa wafanyabiashara kutoka nje ili muweze kukuza biashara zenu, itumieni Tantrade kufanikisha biashara zenu kwa kutazama fursa zilizopo kwenye masoko ya kimataifa,” amesema
Amesema Mwaka 2023 Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilisajili miradi 504 yenye thamani ya dola za Marekani Bilioni 5.68 hii ni kwa sababu watu wanakuja Tanzania wanaona maonesho hayo na kuvutiwa kuwekeza.
Naye Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi akifungua Maonesho hayo amesema kuwa anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuisaidia nchi yake katika kupambana na suala la ugaidi ambalo amelitaka kuwa lilikuwa linazorotesha uchumi wa nchi hiyo.
Rais Nyusi amesema Tanzania imesimama pamoja na watu wa Msumbiji kipindi chote mpaka sasa hali katika nchi hiyo imetulia.
Amesema utulivu na amani ni muhimu kwa matumizi ya fursa za nishati kati ya nchi hizo mbili zenye akiba kubwa ya gesi asilia katika mkoa wa Mtwara na Jimbo la Delgabo Msumbiji.
Aidha amesema katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ambayo ni kati ya mwaka 2018 na 2023 jumla ya biashara za nje za nchi hizo mbili katika uagizaji na mauzo ya nje yalifikia dola za Marekani Milioni 250 tu.
“Hata hivyo uwekezaji kutoka Tanzania kuja Msumbiji zilikuwa Dola za Marekani Milioni 143 tu hiyo ni kati ya mwaka 2013 hadi 2023, ukiangalia kwa makini maonesho haya yatasaidia kuchochea kukuza ukuaji wa kiuchumi na biashara katika nchi zetu hizi mbili,” amesema
Aidha amesema Msumbiji na Tanzania zinaweza kushirikiana katika sekta ya utalii kwani vivutio vilivyopo katika nchi zote mbili vinafanana.
Amesema maonesho hayo yatatumika kama chombo cha kukuza fursa za nchi hizo mbili za ushirikiano katika maeneo ya biashara pamoja na kuanzisha ubia wenye manufaa kwa wawekezaji kutoka Msumbiji na Tanzania.
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omary Saidi Shabani, amesema maonesho hayo yamepata bahati ya kuwa na marais wawili, huku akisema washiriki wote ni 3846 wa ndani ni 3433 huku akisema kuwa maonyesho hayo yamejumuisha nchi 26 kulinganisha nchi 19 za mwaka jana zikiwemo za Afrika na Ulaya.
Amesema washiriki hao kutoka nje ya nchi, wamefika kuonyesha Teknolojia mbalimbali, huku akitaka Watanzania kuendelea kushiriki na kujifunza kupitia maonyesho hayo.
Amesema kuwa, Wizara inaendelea kufanya ukarabati wa barabara za ndani ya maonyesho, kujenga jengo la kisasa la maonyesho, kuandaa mikutano na kuboresha Teknolojia huku akiahidi kuendelea kuboresha maeneo ya biashara.
Kwa upande wa masoko, amesema wanaendelea kuweka mkazo katika masoko ikiwemo fursa ya soko huru Afrika, huku akisema kuwa wizara imeendelea kutekeleza mfumo wa dirisha moja ambao utaanza kufanya kazi mwaka huu.
Awali Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, maonesho hayo yamekuwa yakikua kila mwaka kutoka na ukubwa wake ambapo kwa mwaka jana walifika washiriki 3500 huku mwaka huu imeongezeka ambapo hadi jana walikuwa wamefika washiriki 3846.
Amesema tukio hilo linaonesha ambavyo nchi zote mbili zinathamini maendeleo ya biashara ambapo jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika huku akiwakaribisha wananchi na waoneshaji kupata maarifa na masoko ya biashara na kuongeza juhudi zaidi.