NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Latifa Khamis amesema kuwa tangu kuanza kwa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) Juni 28 mwaka huu hadi leo zaidi ya ajira 17,000 zimepatikana na zitaendelea kuwepo hadi pale yatakapoisha Julai 13, 2024.
Ameyasema hayo leo Julai 3,2024 jijini Dar es Salaam wakati akieleza vitu vilivyofanyika wakati wa maandalizi ya maoneshi ya 48 ya kimataifa ya Dar es Salaam mbele ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi.
Amesema kupitia Maonesho hayo watanzania wengi wamefaidika katika sehemu ajira na kwamba yamekuwa ni nyenzo muhimu ya kupunguza uhaba wa dola zisizopungua 433,889 kwa kipindi chote cha maandalizi pamoja na kufanikisha ukusanyaji wa kodi kutoka kwa washiriki.
“Washiriki wote hawa wanalipia kodi kwa serikali, Tantrade tunakuvika pete ya mafanikio Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha unaweka mazingira mazuri na rafiki kufanikisha maonesho haya,” amesema
Aidha amesema katika kuleta upekee wa maonesho hayo wanamshukuru mdhamini mkuu kwa kuboresha mabanda matatu yenye majina ya viongozi wakuu wastaafu ambayo yameokoa Sh. Bilioni moja ambazo zingetumiwa na mamlaka kukodisha miundombinu wakati wa maonyesho.
“Fedho hizi zimeokolewa kutokana na ufadhili wetu mkuu ambaye ni Kituo cha Kuendeleza Biashara cha Afrika Mashariki (EACLC), fedha hizo sasa zitatumika katika shughuli nyingine,” amesema
Hata hivyo amesema wamezindua rasmi leo program ya Sabasaba urithi wetu kwa kwaleta watoto kutoka mikoa mitano ya Tanzania ili kuweza kujifunza kinachofanyika katika maonesho hayo.
“Programu hii inalenga kuwarithisha watoto hawa mambo yanayofanyika sabasaba, wakija na kuona jambo hili linakaa kichwani kwao na wanaweza kuijua sabasaba, wanatengeneza historia kubwa kwa kushuhudia maonesho haya,” amesema
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu, Viwanda, biashara, kilimo na mifugo , Deudatus Mnyika, amesema kuwa maonyesho hayo ni kipimo cha maboresho makubwa ya sekta ya viwanda na biashara ambapo Kampuni 3280 yameshiriki yakiwemo ya ndani ya nje ya nchi.
Kuhusu Kituo cha Uwekezaji wa EACLC kilichopo Ubungo, amesema mradi huo umeshatoa ajira 2500 huku ajira 15,000 ni za moja kwa maja na ajira 50,000 zisizo za moja kwa moja ambapo alimkaribisha Rais Dk.Samia katika ufunguzi wa kituo hicho.
Akitoa salama za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliwapongeza viongozi kwa kutembea kilometa 13 wa miguu katika maonyesho hayo, jambo ambalo limeonyesha uimara wao na kuleta hamasa zaidi katika maonyesho hayo.
Amesema kuwa, Wananchi wa Mkoa huo, wamefarijika sana kwa namna anavyoimarisha diplomasia ya mataifa mbalimbali ikiwemo Msumbiji ikiwa ni njia ya kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi.
Amesema kuwa, wamejipanga vyema kuhakikisha suala la usalama linakuwepo ulinzi wakutosha kuendelea kuboresha na kuhamasika kushiriki huku akiwa vutia wananchi wengi kushiriki.
Chalamila amesema zaidi ya nchi 26 zimeshiriki katika maonyesho hayo ikiwa ni matunda ya kuimarisha kwa deplomasia, huku akimkaribisha Rais Nyusi kupata makazi katika Mkoa huo na kufanya uwekezaji Zanzibar ambako ameandaliwa eneo maalumu.
Amesema kuwa mkutano huo umeudhuriwa na Mawaziri na Manaibu Mawaziri wa Tanzania, Msumbiji na Zanzibar na viongozi mbalimbali wa wizara, Taasisi, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wakuu wa Taasisi na Mabalozi, Mkuu wa Kituo Cha Afrika Mashariki.