NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewataka Wafanyabiashara nchini kusajili Majina ya Biashara zao ili kupata ulinzi wa kisheria na kuzuia mtu mwingine kuyatumia katika kuendesha biashara.
Hayo yamebainishwa mkoani Morogoro na Mkuu wa Sehemu ya Kampuni kutoka Kurugenzi ya Kampuni na Majina ya Biashara wa BRELA Lameck Nyange wakati akiwasilisha mada iliyohusu majina ya biashara na umuhimu wa kusajili katika mafunzo ya siku nne yanayotolewa na BRELA kwa waandiishi wa habari.
Amesema wapo wafanyabiashara ambao majina ya biashara zao ni maarufu lakini hawajayasajili hivyo kuna watu wanaingia katika mfumo na kisha kusajili na anapokuja mhusika kutaka kusajili anakuta tayari jina limesajiliwa.
Nyange amesema ili mtu haweze kupata ulinzi wa kisheria ni muhimu kuwa amesajili jina lake la biashara na mtu mwingine akilitumia ni rahisi kumshtaki mahakamani.
“Ndio maana BRELA tumekuwa tukitoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kusajili jina la biashara kwani tunalo daftari lenye orodha ya majina yote ya biashara na kampuni ambazo zimesajiliwa. Hivyo mtu anapokuja kusajili tunaingia kwenye mfumo na kuangalia kama tayari jina hilo la biashara limesajiliwa au laa.
“Kuna faida nyingi za mfanyabiashara kusajili jina la biashara na moja ya faida kubwa ni ulinzi wa jina lake maana BRELA tunaposajili jina la biashara tunalilinda na hivyo linakuwa katika ulinzi na kwa mwaka gharama ya jina la biashara ni Sh.5000 tu. Sajilini majina yenu ya biashara kwani hata mtu mwingine ukikuta amelitumia ni rahisi kwenda kushitaki mahakamani,” amesema Nyange.
Akifafanua zaidi amesema faida nyingine ya kusajili jina la biashara ni mfanyabiashara kupata fursa mbalimbali zikiwemo za kifedha kama kupata mkopo.
“Lakini faida nyingine mtu anakuwa amefanya biashara muda mrefu na amekuwa maarufu lakini kwasababu hujasajili mtu mwingine anasajili, hivyo unasajili, hivyo hakuna anayeweza kusajili tena,” amesema Nyange