NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema kuwa katika kuhakikisha inakwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ikiwa ni pamoja na kurahisisha zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura imeboresha mfumo wa uandikishaji.
Imesema mfumo huo ulioboreshwa kwa mara ya kwanza utamuonesha Mpiga Kura aliyekuwepo kwenye daftari kuanzisha mchakato wa kuboresha ama kuhamisha taarifa zake kwa kutumia simu ya mkononi au kompyuta na baadaye atakamilisha mambo mengine yanayohitajika ikiwemo na kupiga picha.
Hayo yamebainishwa hayo leo Juni 15,2024 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Uchaguzi INEC, Ramadhani Kailima wakati akifungua mkutano wa Tume hiyo na Maofisa Habari wa Mikoa na Halmashauri za Tanzania Bara kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Amesema Maofisa Habari wa Mikoa na Halmashauri wana jukumu la kuwaelimisha na kuhabarisha wananchi wakiwemo walemavu ili kupata uelewa wa kutosha kuhusu uboreshaji na hatimaye wajitokeze kwa wingi kujiandikisha.
“Lengo la kukutana nanyi ni kuendelea kuwakumbusha kuwa mnajukumu kubwa la kuwahabarisha umma ili waweze kujitokeza kwa wingi katika zoezi hili la uboreshaji wa daftari ambalo litaanza Julai Mosi mwaka huu.
“Aidha nawaomba wadau mbalimbali wa uchaguzi wazingatie sheria za Uchaguzi, kanuni za uboreshaji na maelekezo ya tume, kwa upande wa Maofisa wa Tume watazingatia Sheria za uchaguzi katika zoezi hili,” amesema
Kailimia pia amewataka Waandishi wa Habari kupinga aina yeyote ile ya upotoshwaji ili kurahisisha kazi hiyo kufanyika kwa uzuri na ufanisi mkubwa.
Amesema INEC inatarajia kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Maofisa Habari hao ambao wanafanya kazi kubwa ya kuhabarisha umma katika mikoa na Halmashauri wanazofanyia kazi.