*Sababu ni kutofanya vizuri,kupitwa na wakati
*Prof.Mkumbo asema kwa sasa hayana umuhimu
* Awataka Wakuu wa Mashirika hayo kuwa tayari
NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema yapo Mashirika ya Umma 14 ambayo yataunganishwa na mengine manne kufutwa kutokana na kutofanya vizuri ama kupitwa na wakati.
Prof. Mkumbo aliyasema hayo leo Juni 11,2024 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuhusiana na utekelezaji wa zoezi la kuyafuta ama kuyaunganisha Mashirika hayo yasiyofanya vizuri ama kupitwa na wakati.
Amesema wanatekeleza maagizo hayo wakiongozwa na ukweli kwamba yapo Mashirika ya Umma yaliyoanzishwa miaka ya 70 na 80 yalikuwa muhimu sana kipindi hicho lakini sasa hivi umuhimu wake hama haupo au umepungua hivyo tutamshauri Rais hayafute.
“Lakini yapo mashirika ya umma ambayo majukumu yake yanaingiliana sana hivyo tutamshauri Rais kuyaunganisha na tumefanya hivyo kwahiyo yapo 16 yataunganishwa, mchakato huu utaboresha mazingira ya biashara na uwekezaji” amesema Prof. Mkumbo
Prof. Mkumbo amesema Wenyeviti wa bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika hayo wawe tayari ama mmoja kubaki katika nafasi hiyo ama wote kuondolewa kama ambavyo itampendeza mwenye Mamlaka ya uteuzi.
Aidha amesema kuwa ili kuyafanya mashirika ya umma yawe na umiliki wa wananchi, serikali inakamilisha mchakato wa kuyaandikisha kwenye soko la hisa ili wananchi wanunue hisa na wayamiliki.
Amesema wapo katika hatua za mwisho kukamilisha zoezi hilo na hivi karibuni watatoa taarifa.
Naye Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu amewataka Watendaji wakuu na Wakurugenzi wa Mashirika hayo ya Umma wawe tayari kwa mabadiliko yatakayosaidia kubadili namna yao ya kuendesha mambo na kutoa gawio kwa serikali.
Amesema ni muhimu pia Watendaji wa Mashirika hayo kuongeza ubunifu na kukuza mapato ya taasisi zao ili yaweze kuingia kwenye mfumo mkuu wa serikali na kusaidia katika maendeleo ya Taifa.