NA MWANDISHI WETU
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) wamesaini makubaliano na taasisi nne za Serikali wakikubalina kushirikiana ili kuleta ufanisi chanya hapa nchini.
Taasisi ambazo zimesaini makubaliano na Brela jijini Dar es salaam leo Mei 9, 2024 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Miliki Duniani ni Chuo Cha Mzumbe, TIA na Mamlaka ya Afya ya Viwatilifu (TPHPA) .
Katika maadhimisho hayo, ambayo yamefanyika hapa nchini, Duniani kote ikiwa imefanyika Aprili 26, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sana na Michezo, Hamisi Mwinjuma (Mwana FA) akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara Ashatu Kijazi, amewataka Brela na Cosota kutoa elimu zaidi hususani kwa wabunifu ili wanafuike na kazi zao.
“Niwaelekeze Brela na Cosota wakae Kwa pamoja waangalie namna ya kutoa wabunifu wakiwemo wasanii wachanga ili kutoa fursa ya kunufaika na kazi zao kutokana na elimu watakayokuwa nayo kuhusu Miliki Bunifu”, amesema.
Aidha ameongeza kuwa Brela wanatakiwa kuhakikisha wanajielekeza kuifanyia Miliki Bunifu inatambulika na wabunifu waweze kukopesheka tofauti na hivyo inaweza kutafsirika kama porojo.
Pia ameipongeza Taasisi ya Ruge Mutahaba kuja na wazo la kupeleka elimu ya Miliki Bunifu kwa wasanii wadogo ambapo pindi watakapoelimima wataweza kuweka ulinzi kwenye kazi zao.
“Katika siku hii ya leo ni vema kupitia majadiliano yenu mnapata majibu ya changamoto zilizoko na kuziwasilisha wizarani kwa ajiliya kufanyiwa kazi ili tutakapokutana tena mwakani tuwe na jambo lingine la kufanya na si kurejea haya,” amesema.
Pia amebainisha kuwa Wizara inaendelea kufanya Mchakato wa kukamiisha sera ili kutoa mchango mkubwa katika sekta Bunifu.
Pia Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela Godfrey Nyaisi, amesema kuwa elimu kuhusu Miliki Bunifu bado iko chini nchini hivyo wanaendelea kuelimu ili kufanikisha lengo husika.
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha wanafikia malengo wamekuwa na utaratibu wa kutoa ufadhili kwa wafanyakazi wao kuendeleza na masomo ya katika kozi ya Miliki Bunifu ndani na nje ya nchi.
Katika shughuli hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Nyaisa na Naibu Waziri, Mwinjuma walikabidhi mfano wa hundi Kwa wanufaika wanne wa masomo ya Miliki Bunifu ya sh. Milioni 16.5 Kwa kila moja.




Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri Brela, Neema Mboya, amesema kuwa wataendelea kusimamia vema taasisi ili ilete ufanisi katika shughuli zake na kupata mafanikio stahiki.
Ameongeza kuwa baadhi ya mafanikio ambayo yamepatikana katika kipindi hiki ni nchi za Burundi na Sudani Kusini kuja hapa nchini kuja kujifunza mifumo inayotumiwa na Brela kwenye shughuli zake na kupata matokeo chanya.
Ameongeza kuwa mataifa hayo baada ya kujifunza wamekwenda kuifanyia kazi nchini ili kuondoa changamoto baina yao na wafanyabiashara.
Aidha amefafanua kuwa baadhi ya sheria zinazoongoza Brela zimepitwa na wakati hivyo zinaendelea kufanyiwa kazi ili kuleta ufanisi wenye tija nchini.