NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
MABALOZI iwa Nchi za Umoja wa Ulaya wametembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo(SUA) ili kujionea miradi mbalimbali inayoendelea chuoni hapo kwa ufadhili wa Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo.
Mabalozi hao wakiongozwa na Balozi wa Jumuiya ya Ulaya na Jumuiya ya Afrika Mashariki Christine Grau, wamepokelewa chuoni hapo na Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda na kupata fursa kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Chuo.
Katika ziara hiyo Mabalozi wametembelea Kituo cha Kitaifa cha Kufuatilia Kaboni SUA, na kupata maelezo kuhusu kituo hicho kinavyofanya kazi kutoka kwa Mkurugenzi wa Kituo hicho, Prof. Eliakim Zahabu ambaye ameeleza namna kituo kinavyopokea maandiko mbalimbali kutoka kwa taasisi na watu binafsi wakieleza namna wanavyoweza kubuni shughuli rafiki kwa mazingira ili kupunguza athari za Mabadiliko ya Tabia ya Nchi.
Kwa upande wa Kituo cha Kufundishia Panya (APOPO), Mabalozi wameweza kujionea namna panya wanavyotumika kugundua vitu vilivyofichwa ardhini.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, upande wa Mipango , Fedha na Utawala, Profesa Amandus Muhairwa, amesema Mabalozi hao wameridhika na kinachofanyika SUA na hivyo kuweza kuendelea na mahusiano wakiwa ni wafadhili wa miradi mbalimbali inayotelezwa .
“Hii imekuwa ni nafasi ya kuonesha tuliyoyafanya na kuendeleza mahusiano wakiwa ni wafadhili kwa faida ya nchi na faida kwa vijana ambao ni wanufaika katika kutengeneza ajira ambalo ni lengo la miradi hii mingi inayofanyika chuoni” alizungumza Profesa Muhairwa.
Kiongozi wa Mabalozi, Grau amesema, wamefurahishwa na maendeleo ya miradi inayofanywa SUA.
Pia amewataka vijana wa Kitanzania ambao wamepata fursa ya kufikia Elimu ya Juu kutumia muda wao vizuri ili waweze kufaulu masomo na kututua changamoto za jamii wanazotoka ikiwepo suala la Athari ya Mabadiliko ya Tabia ya Nchi.