NA MWANDISHI MAALUMU, DAR ES SALAAM
TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) inatarajia kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto 500 katika kipindi cha mwaka mmoja yatakayogharimu Sh. Bilioni 1/-
Fedha hizo zinatarajiwa kukusanywa Julai 6, mwaka huu, kupitia chakula cha jioni (Dinner Gala) itakayofanyika jijini Dar es Salaam katika Hoteli ya Johari Rotana chini ya shirika lisilo la kiserikali la Heart Team Africa Foundation (HTAF) linaloshughulika na upatikanaji wa matibabu ya moyo kwa watoto wasio na uwezo.
Akieleza kuhusu mpango huo wa kuwatibia watoto hao leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dk. Peter Kisenge alisema lengo la kutoa matibabu hayo ni kuokoa maisha ya watoto waliozaliwa na mgonjwa hayo kupitia HTAF na Tasisi hiyo.
“Takwimu zinaonesha kuwa watoto wengi wanazaliwa na matatizo ya moyo kati ya watoto milioni mbili wanaozaliwa kwa mwaka 14,000 wamakuwa na matatizo ya moyo na watoto 4,000 wanahitaji upasuaji”, amesema Dk Kisenge.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alieleza kwamba JKCI kwa mwaka uliopita ilifanya upasuaji wa moyo kwa watoto 357 ambapo kwa mwaka huu wanataraji kufanya upasuaji kwa watoto 500.
Alisema kupitia Sh.Bilioni 1 inayotarajiwa kukusanywa na HTAF, itawezesha kuwatibia watoto hao, hususan wale wa vijijini ambao hawana uwezo wa kugharamia huduma hizo.
Mkurugenzi huyo mtendaji Dkt. Kisenge alisema gharama za matibabu ya moyo kwa watoto ni ghali hadi kufikia Sh. Milioni 10 kwa mgonjwa mmoja na Sh. Milioni 15 kwa upasuaji wa mtoto mmoja, huku wakiishukuru serikali na wadau mbalimbali kwa kudhamini watibabu hayo.
Dk. Kisenge aliishukuru serikali kwani imekuwa ikifadhili matibabu ya watoto kwa sehemu kubwa, karibu asilimia 70 hadi 90, kwani walio wengi hawawezi kumudu gharama hizo.
Kaimu mtendaji Mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Heart Team Africa Foundation (HTAF),Linda Gideon alisema lengo kuu la kuanzishwa kwa shirika hilo ni kuboresha huduma za moyo kwa jamii ndani na nje ya Tanzania.
“Pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali kuchangia matibabu kwa asilimia 70 bado kuna changamomoto ya kumalizia kiasi kilichobaki na ili kufanikisha hilo tumeandaa chakula cha jioni hoteli ya Johari Rotana tutashirikiana na jamii”.
“Tunaomba wadau wote ambao wanawiwa kusaidia watoto wajitokeze kwa wingi kurudisha tabasamu la watoto wenye tatizo la moyo na tutatoa account maalumu kwa watu wanaotaka kuchangia wataweka katika akaunti hiyo”, amesema Linda.
Akielezea kuhusu hafla hiyo ya chakula cha jioni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa JKCI Naizihijwa Majani amesema wamejipanga vyema kuhakikisha wanafanikisha harambee hiyo kupitia fedha hizo za kuwatibia watoto.
Alisema kuwa katika usiku huo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Mstaafu Dk Jakaya Mrisho Kikwete, hivyo aliwaomba watu wajitokeze kwa wingi ambapo watatangaza utaratibu maalumu utakaotumika.
Kwa upande wake, Meriselina Athanasi ambaye ni mama mzazi wa mtoto mwenye ugonjwa wa moyo aliishukuru serikali kupitia JKCI kwa namna ambavyo imewasaidia kupata matibabu bila gharama.
Alisema kuwa, baada ya kugundua tatizo hilo kwa mtoto wake, ndugu zake walidai hawana uwezo wa kumsafirisha wala kumtibu mtoto huyo hivyo wasamalia wema walimpatia nauli ya kufika Dar es Salaam akitokea Morogoro.
“Ninamshukuru Mungu mtoto wangu baada ya kufanyiwa vipimo anaendelea vizuri sasa hivi tuko wodini anasubiria kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo, nimepewa gharama ya upasuaji ni milioni nane ”.
“Gharama ya upasuaji ni kubwa mimi peke yangu siwezi kulipia, tunaiomba Serikali na wananchi msituchoke mtusaidie kulipia gharama za matibabu ya moyo ya watoto wasiokuwa na uwezo”, alisema Theochrista Kambi mama wa mtoto mwenye shida ya moyo.