NA TERESIA MHAGAMA,DODOMA
NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema kuwa, Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) itaendelea kuongeza bajeti
kila mwaka ya matengenezo ya miundombinu ya umeme hadi changamoto ya
kukatika umeme kutokana na uchakavu wa miundombinu ya kusafirisha na
kusambaza umeme itakapoisha kabisa.
Naibu Waziri Kapinga ameeleza hayo 23 Aprili 2024 bungeni
jijini Dodoma wakati akijbu swali la Mbunge wa Jimbo la Segerea,
Bonnah Kamoli aliyetaka kujua ni lini changamoto ya kukatika kwa umeme
mara kwa mara itaisha nchini.
”Changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini inatokana na
uchakavu wa miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme, miundombinu
hiyo inahitaji uwekezaji mkubwa sana hivyo Serikali kupitia TANESCO
imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kukarabati miundombinu hii na kwa
mwaka wa fedha 2023/24, Serikali kupitia TANESCO imetumia jumla ya
shilingi 109,896,003,751 kwa ajili ya kuboresha miundombinu husika.”
alisema Kapinga
Aliongeza kuwa, Serikali pia imetumia jumla ya shilingi
105,515,860,225 katika miradi ya kuimarisha nguvu ya umeme Tanzania
(Voltage Improvement projects) na kwa sasa, TANESCO imeanza kutumia
nguzo za zege ambazo zinadumu kwa muda mrefu zaidi.
Akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Charles Kimei
aliyetaka kujua lini umeme wa REA utafikishwa katika Kata zote Jimbo
la Vunjo, Mhe. Kapinga amesema kuwa vijiji vyote 78 kwenye Kata 16 za
Jimbo hilo vimesambaziwa umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini
(REA) pamoja na TANESCO.
Aliongeza kuwa, katika vitongoji 301 vya Jimbo hilo tayari vitongoji
260 vimepatiwa umeme na katika mwaka 2023/24, Serikali kupitia Wakala
wa Nishati Vijijini utapeleka umeme katika vitongoji 15 vya Jimbo la
Vunjo na hivyo kusalia na vitongoji 26 ambavyo kazi ya kuvipelekea
umeme itaendelea kuratibiwa na REA kulingana na upatikanaji wa fedha.