NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema ni wajibu kuulinda Muungano, kuuendeleza, kuudumisha na kuimarisha zaidi ili kuzidi kunufaika kwa dhamira ile ile ya Waasisi wa Taifa letu.
Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa umoja wa Watanzania unazidi kuimarika , ushirikiano katika shughuli mbalimbali unaongezeka na amani inaendelea kudumu nchini.
Rais Dk.Mwinyi amesema hayo alipofungua Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Maonesho ya Taasisi mbalimbali viwanja vya Nyamanzi , Mkoa wa Mjini Magharibi Aprili 14 ,2024.
Aidha Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuzitafutia ufumbuzi changamoto zote zinazojitokeza katika utekelezaji wa masuala ya Muungano.
Halikadhalika Rais Dk.Mwinyi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuweka vipaumbele masuala ya kuimarisha Muungano.
Rais Dk.Mwinyi amesema Tanzania imefikia mafanikio makubwa kipindi cha Miaka 60 katika nyanja zote za maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na huduma za jamii.
Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi amewahimiza wananchi kuendelea kushiriki shamrashamra za sherehe za miaka 60 ya Muungano katika Mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar ikiwa ni pamoja na siku ya kilele Aprili 26,2024 katika uwanja wa Uhuru Dar es Salaam ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Dk.Samia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais Dk.Mwinyi amesema kipindi cha miaka mitatu, 2021 hadi mwaka 2024 hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 18 zilizokuwepo.
Vilevile Rais Dk.Mwinyi amesema Tanzania imeendelea kubaki katika historia na mfano bora wa kudumisha Muungano barani Afrika na duniani kote.