*Akagua mabwawa ya Kihansi na Kidatu
*Akuta mabwawa yamejaa maji, asema changamoto ya umeme ipo ukingoni
*Akataza Likizo kwa watendaji kipindi cha changamoto za umeme
*Amshangaa Meneja aliyeenda likizo kipindi cha changamoto*
*Aweso awataka watendaji waondokane na utendaji wa kimazoea
NA TERESIA MHAGAMA, MOROGORO
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko
ameendelea na ziara ya kukagua vyanzo mbalimbali vya uzalishaji umeme
nchini ambapo leo amekagua Bwala la kuzalisha umeme la Kidatu ( 204
MW) na Kihansi ( 180 MW) mkoani Morogoro.
Lengo la ziara hiyo ni kujihakikisha hali halisi ya uwepo wa maji
kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme nchini pamoja kukagua mitambo ya
kuzalisha umeme.
Baada ya kukagua Bwawa la Kidatu na Kihansi pamoja na mitambo ya
kuzalisha umeme, Dkt. Biteko amesema kuwa, mabwawa ya Mtera, Kihansi
na Kidatu yana maji ya kutosha kuweza kuzalisha umeme huku tumaini
jingine kubwa likiwa ni umeme kutoka mradi wa Julius Nyerere (JNHPP)
ambao muda wowote unatarajia kuingiza megawati 235 katika Gridi ya
Taifa.
“Nafurahi kuwaambia kwamba changamoto tuliyonayo ya umeme imefika
mwishoni sana hivyo Watendaji wa TANESCO ni wakati pia wa
kushughulikia changamoto nyingine ambazo baadhi ya wananchi wanazipata
ikiwemo ya kutotoa huduma kwa wakati na pia ukarabati wa mitambo
ufanyike kwa wakati.” amesema Dk Biteko
Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amekataza Watendaji wa TANESCO
kwenda likizo kipindi cha changamoto za umeme na badala yake wajikite
katika kutatua changamoto hizo na katika hilo ameagiza Uongozi wa juu
wa TANESCO kumchukulia hatua za kinidhamu Meneja wa TANESCO Mkoa wa
Morogoro ambaye amechukua likizo katika kipindi hiki ambacho Serikali
inapambana kutatua changamoto za umeme.
” Niliposema TANESCO hamtolala kipindi cha mgawo wa umeme nilimaanisha
kuwa kila mtu awepo kwenye kituo chake cha kazi, sisi wenyewe
tunahangaika kutatua changamoto za umeme halafu baada ya kufika hapa
nimeshangazwa kuona Meneja wa Mkoa ambaye alipaswa kuwepo kituoni
wakati wa changamoto amechukua likizo, hivyo nimewaelekeza watendaji
wa TANESCO hakuna kwenda likizo kuanzia sasa.” amesema Dk. Biteko
Amesema kuwa, Rais, Dk Samia Suluhu Hassan ametoa kila rasilimali
kwa ajili ya kuwapatia watanzania umeme hivyo viongozi na watendaji wa
Wizara hawatakuwa kikwazo cha kumkwamisha.
Ameeleza kuwa, kwa sasa kutakuwa na ushirikiano kati ya Wizara ya
Nishati na Wizara ya Maji katika kulinda vyanzo vya maji na kwamba
itatengenezwa timu ya pamoja ya Serikali kuhakikisha kwamba vyanzo
vyote vya maji vinavyoleta umeme vinalindwa kwa gharama yoyote na wote
wanaovamia vyanzo hivyo watachukuliwa hatua.
Vilevile. Dk.Biteko ameiagiza TANESCO kuhahakisha kuwa wakazi
wanaozunguka Bwawa la Umeme la Kidatu wanapatiwa umeme wa uhakika ili
waone faida ya kulitunza bwawa hilo kimazingira na pia kuwa walinzi wa
Bwawa hilo.
“Wakazi wa Kilombero walioko karibu na bwawa hili waondolewe kwenye
mgao, haiwezekani wao wanalitazama na kulinda bwawa, lakini hawana
umeme; alisema Dkt. Biiteko na kuwaelekeza wataalam kuumiza vichwa na kuja na mwarobaini.
Kuhusu suala la maji kukatika kwenye baadhi ya maeneo ambapo Mamlaka
za Maji zimekuwa zikisema kwamba sababu ni changamoto ya umeme huku
wakati mwingine umeme ukiwepo, Dkt. Biteko ameelekeza kuwa umeme usiwe
chanzo cha kujificha kwenye utendaji kazi na kwamba kila mtu ajikite
kwenye kutoa huduma bora kwa watanzania.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewataka watendaji
wa Sekta za Nishati na Maji kuacha visingizio wakati wa utendaji kazi
na wasizoee shida za wananchi na kuongeza kuwa sekta hizo
zinategemeana hivyo ni lazima zishirikiane.
Amesema kuwa, Wizara yake, kupitia mabonde ya Maji yote tisa watakuwa
mstari wa mbele katika kutunza na kulinda rasilimali ya maji.
Ameongeza kuwa, suala la utunzaji na ulindaji wa vyanzo vya maji ni
jambo shirikishi hivyo Wizara ya Maji na Wizara nyingine kama Mifugo,
Nishati na Mazingira lazima zishikamane kulitekeleza.
Pia ametaka Maofisa katika Mabonde ya Maji nchini kutokukaa maofisini
bali jukumu lao ni kusimamia vyanzo vyote vya maji kwa ukaribu na
washirikishe wananchi na viongozi kwenye maeneo wanayosimamia.
—