NA MWANDISHI MAALUMU, DAR ES SALAAM
KAMATI ya kudumu ya bunge ya Afya na masuala ya Ukimwi imelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kukamilisha haraka mradi wa ujenzi wa jengo la utawala na vipimo la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dk. Faustine Ndugulile Mbunge wa Kigamboni wakati wa ziara ya kamati hiyo waliyoifanya JKCI kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Dk.Ndugulile amesema katika ziara hiyo wametembelea maeneo mbalimbali ya Taasisi hiyo, wamezungumza na wagonjwa ambao wanafurahia huduma wanazozipata na kuona huduma zinazotolewa lakini wamekutana na changamoto ya ufinyu wa miondombinu katika eneo la kusubiria wagonjwa, eneo la vipimo na vyumba vya kulala wagonjwa.
“Tanzania tunayotaka kwenda nayo siyo ya wagonjwa kulala wengi katika chumba kimoja kwani dunia inakoelekea kila mgonjwa aliyelazwa hospitali atalala katika chumba chake ninaamini kukamilika kwa jengo hili la ghorofa nne kutasaidia kupunguza changamoto ya nafasi katika Taasisi hii”.
“Kazi hii ya ujenzi imechukuwa muda mrefu kukamilika ilibidi ikamilike mwezi wa tano mwaka jana lakini hadi sasa ujenzi bado haujakamilika na malipo yao yako tayari, ninaiagiza wizara ya afya wafanye kazi kwa ukaribu ya kusimamia watu waliopewa kazi hii ili wakamilishe mapema na huduma ianze kutolewa”, amesema Dk.Ndugulile.
Aidha kamati hiyo imeridhika na huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa JKCI kwani imefanya mapinduzi makubwa ndani ya miaka 10 asilimia 90 ya wagonjwa waliokuwa wanapelekwa nje ya nchi kutibiwa hivi sasa wanatibiwa hapa nchini na aslimia 95 ya wagonjwa wa moyo wanatibiwa hapa nchini.
Dk.Ndugulile amesema kupatikana kwa huduma bora za kibingwa za matibabu ya moyo hapa nchini kumewafanya wagonjwa kutoka nje ya nchi kuja kuibiwa na hivyo kuhamasisha utalii wa matibabu.
Alimpongeza Rais wa awamu ya sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha huduma za matibabu ya moyo hapa nchini kwa kuboresha majengo, kusomesha wataalamu na kununua vifaa tiba vya kisasa.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy Mwalimu aliishukuru kamati hiyo kwa kufanya ziara yao katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kujionea kwa macho huduma wanazozitoa, kuzungumza na wagonjwa pamoja na kufahamu changamoto zilizopo.
Ummy amesema katika nchi za Afrika ukiondoa Afrika ya Kusini na Misri Tanzania inafanya vizuri katika matibabu ya moyo. Hivi karibuni alikutana na wadau wa afya kutoka nchini Marekani ambao walisema watashirikiana na JKCI na kuhakikisha inakuwa kituo kikubwa cha matibabu ya moyo barani Afrika ila waliomba huduma hizo zisambae zaidi mikoani .
“Ili kusogeza huduma za kibingwa za matibabu ya moyo karibu na wananchi ni muhimu JKCI ikaanzisha matawi mikoani katika kanda zote lakini kipaumbele kiwe kanda ya ziwa katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato ili wataalamu wajengewe uwezo na kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo na wananchi wengi zaidi watafikiwa na huduma hizo”, amesisitiza Ummy.
Aidha Ummy amesema wataalamu wa afya wamekuwa wakifanya kazi nzuri ya kuokoa maisha ya wagonjwa ila inapotokea changamoto kidogo katika utoaji wa huduma wamekuwa wakilaumiwa jambo ambalo linawavunja moyo, lakini wizara imekuwa ikiwachukulia hatua wale wote wanaokwenda kinyume na kanuni na miongozo ya matibabu.
”Ninaomba tuwatie moyo wataalamu wa afya tusiwavunje moyo kwani kazi wanayoifanya ni ngumu tukiwatia moyo wataona tuko pamoja na tunawajali, kuna baadhi ya watumishi wa afya ambao wanafanya kazi zao kinyume na maadili hawa wote Wizara imekuwa ikiwachukulia hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kuwafutia leseni”, amesema Waziri Ummy.
Waziri huyo wa Afya alisema kuanzishwa kwa huduma ya afyamtandao (telehealth) katika Taasisi hiyo kutasaidia kupuguza gharama za mgonjwa kusafiri kutoka mkoani na nje ya nchi kufuata huduma ya matibabu Dar es Salaam kwa kutumia huduma hiyo ataweza kufanya consultation na kupata huduma za matibabu na dawa akiwa mbali na Hospitali.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dk. Peter Kisenge alisema Taasisi hiyo imekuwa ikihudumia wastani wa wagonjwa 400 hadi 500 kwa siku huku wagonjwa wanaolazwa wastani wake ukiwa ni 100 kwa wiki.
Taasisi hiyo inatibu wagonjwa kutoka nje ya nchi huku wengi wao wakiwa ni kutoka katika nchi za Malawi, Kongo, Zambia, Rwanda, Burundi, Visiwa vya Comoro, Kenya, Msumbuji, Burundi pamoja na kutoka nchi za nje ya Bara la Afrika ambao wanakuja hapa nchini kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo za utalii .
“Ili kusongeza huduma kwa wananchi tumekuwa tukitoa huduma ya tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwafuata wananchi mahali walipo na kuwapa elimu ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kufanya upimaji na matibabu ya moyo ambapo hadi sasa tumetembelea mikoa 12”.
‘Katika mikoa 12 tuliyokwenda kutoa huduma za tiba mkoba tumeona wagonjwa zaidi ya 10000 kati ya hao wagonjwa 2800 hawakuwa wanajijua kuwa na tatizo la ugonjwa wa moyo na wagonjwa 1000 walikutwa na matatizo yaliyohitaji matibau ya kibingwa na tuliwapa rufaa ya kuja kutibiwa JKCI”, amesema Dk.Kisenge.
Dk.Kisenge amesema Taasisi hiyo imekuwa ikipata ushirikiano wa kutosha kutoka Wizara ya afya kwani imekuwa ikiisimamia na kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.