NA HAPPINESS SHAYO,DODOMA
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amesema Serikali itahakikisha inaendelea kutumia teknolojia ya kisasa kwa kadri inavyowezekana kudhibiti wanyama wakali na waharibifu hususani tembo ili kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyamapori.
Ameyasema hayo leo Februari 7,2024 katika kikao chake na Wabunge wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kilicholenga kusikiliza changamoto wanazokabiliana nazo wananchi katika kuthibiti wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo yao kilichofanyika jijini Dodoma.
“Katika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo tunatumia teknolojia ya Geofencing ambapo tutaweza kupata taarifa endapo tembo amesogea karibu na uzio uliowekwa na hivyo askari wetu watachukua hatua za haraka” Kairuki amefafanua.
Pia, Waziri Kairuki amesema Serikali imeanza kutumia teknolojia ya kufukuza tembo kwa kutumia kamera za drones ambapo majaribio ya kwanza yamefanyika katika pori la Akiba la Selous.
Kuhusu uzio wa umeme amesema Serikali inaendelea na majaribio kuona kama njia hiyo inafaa au la ambapo kwa sasa majaribio yamefanyika Pori la Akiba la Grumet.
Aidha, amewahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa Serikali inafanya kila liwezekanalo kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo yao.
“Niwahakikishie tutakapoweza kukodi helikopta tutafanya hivyo, itakapohitajika kutumia helikopta ya kwetu tutafanya lakini kwa sasa tunaangalia tufanye nini kwa kudhibiti wanyama hao kwa kutumia mikakati ya muda mfupi na ya muda mrefu”amesisitiza Kairuki.
Amesema pia Serikali inafanyia kazi madai ya kifuta jasho na kifuta machozi ambapo mpaka sasa uhakiki umeshafanyika hivyo ufuatiliaji wa fedha unaendelea ili wahusika walipwe.
Kuhusu kutangaza vivutio vya utalii vya ukanda wa kusini, Mhe. Kairuki amesema Serikali itafanya tathmini ya kina kuweza kuviibua, kuvitangaza na kuviendeleza vivutio vya utalii vya Ukanda wa Kusini hasa Kilwa Kisiwani na maeneo ya fukwe ya Pangani, Mkinga na Mafia.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Salma Kikwete amesema maeneo mengi ya Mikoa ya Lindi na Mtwara yanakabiliwa na changamoto ya tembo hivyo kuiomba Serikali kutafuta ufumbuzi wa muda mrefu ili kuepuka madhara yanayowapata wananchi hasa kuliwa mazao yao.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula Wabunge wa Mikoa ya Lindi na Mtwara, Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake za Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS)