NA MWANDISHI WETU,DODOMA
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Ukimwi imesema imeridhishwa na utendaji wa Bohari ya Dawa(MSD) na mipango ya utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo uzalishaji wa dawa ili kupunguza kununua dawa nje ya nchi.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI, Stanslaus Nyongo baada ya kupokea taarifa ya hali ya utendaji na majukumu ya Bohari ya Dawa (MSD), ambapo ameichagiza MSD kuongeza ufanisi, ubunifu wa hali ya juu kwa kuhakikisha bidhaa za afya zinakuwa toshelevu na kusambazwa.
Kwa upande mwingine Nyongo ameshauri MSD kufuatilia na kukusanya madeni ili kuhakikisha inajiendesha vizuri bila kuathiri mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya na kuongeza kuwa wataendelea kuishauri serikali kuiwezesha MSD kupata mtaji ili iweze kujiendesha.
“Bohari ya dawa sasa imeongezewa jukumu moja la kuzalisha bidhaa za afya na kuifanya sasa kutekeleza majukumu manne ambayo ni kuzalisha, kununua, kutunza na kusambaza bidhaa za afya katika vituo vya vyote vya umma vya kutolea huduma za afya nchini” ameeleza Nyongo
Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai kwa uongozi imara katika taasisi hiyo na kuwezesha upatikanaji wa bidhaa za afya kuongezeka na kufikisha vituoni kwa wakati.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Tukai ameeleza kuwa tayari wameanzisha kampuni Tanzu ambayo itaingia mikataba na makampuni binafsi ya ndani na nje kuwekeza kwenye viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali za afya nchini, na wajumbe wanne wa Bodi wa kampuni hiyo tanzu wameshateuliwa